Ulimwengu waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinda amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ulimwengu waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinda amani

Serikali ya Tanzania imesema licha ya changamoto zinazoendelea kuvikabili vikosi vyake vya kulinda amani, bado itaendelea kushiriki operesheni za amani kwenye maeneo yenye mizozo

Tanzania ambayo inashiriki opereshini mbalimbali imesema moja ya kipaumbele chake ni kuendelea kusalia mstari wa mbele katika ulinzi wa amani na itaendelea kufanya hivyo kama sehemu ya kuitikia mwito wa taasisi za kimataifa yaani Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika operesheni za kuleta amani.

Imesema ingawa kumekuwa na mikwano ya hapa na pale inayovikabili vikosi vyake, lakini hilo haliwezi kuirudisha nyuma na itaendelea kupeleka walinzi kadri itakapohitajika.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya kuwakumbuka walinzi wa amani, Waziri wa Ulinzi Dk Huseen Mwinyi amesema dunia imeendelea kushuhudia maelfu ya walinda amani duniani wakipoteza maisha na wengi wao wanakumbana na madhila hayo wakati wakitekeleza majukumu ya kujitolea.

Hussein Mwinyi (gemeinfrei)

Waziri wa ulinzi Tanzania Hussein Mwinyi

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba tangu kuasisiwa na shughuli za ulinzi wa amani duniani mnamo mwaka 1948, kiasi cha walinda amani 380 wamepoteza maisha hadi sasa.

Ingawa suala la ulinzi wa amani duniani limekuwa likitiliwa maanani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama wa kudumu watano kupitia maazimio yake, hata hivyo katika ulisia wake,walinda amani wengi wanatoka nchi za Afrika na kiasi fulani katika mataifa ya Asia. Hadi sasa kuna zaidi ya walinda amani 100,000 walitimiza majukumu yao duniani.

Katika kipindi cha mwaka 2017-2018 Tanzania ilipoteza idadi kubwa ya walinda amani kwa kwa wakati mmoja wakati waliposhambuliwa kwenye maeneo yao huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Akizungumza mjini New York, Marekani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya kupokea medali sita za walinda amani waliopoteza amani huko Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Modesti Mello alisema Tanzania bado iko bega kwa bega na Umoja wa Mataifa.

Mbali ya kupeleka walinda amani huko Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Tanzania pia imepeleka vikosi vyake katika mataifa mengine ikiwamo Lebanon na Sudan katika Jimbo la Darfur kwenye mzozo kati ya raia na wapiganaji wa Janjaweed.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com