1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukatili wa kingono kwa watoto na wanawake wakithiri Tanzania

Sylvia Mwehozi
31 Agosti 2018

Ripoti iliotolewa na kituo cha kituo Cha sheria na haki za binadamu inaonesha kuwa matukio ya ukatili wa kingono miongoni mwa watoto na wanawake yameongezeka nchini Tanzania katika kipindi cha nusu mwaka wa 2018. 

https://p.dw.com/p/345RS
Kinder in Tansania
Picha: DW/Z. Mussa

Ripoti hiyo inaonesha kuwa wastani wa watoto mia tatu tisini na nne wamebakwa kila mwezi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania bara, huku ulawiti wa watoto ukiongezeka kwa matukio 12 kwa kipindi cha Januari hadi June 2017, mpaka 533 kwa kipindi cha Januari hadi June 2018, na mikoa inayoongoza zaidi ni Dar es Salaam na Iringa.

Fundikira Wazambi, alieongoza utafiti huo kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu, amewaambia wanahabari kuwa watekelezaji wakubwa wa ukatili huo wanatajwa kuwa ni watu wa karibu na watoto huku wengi wao wakielezwa kuwatishia maisha endapo watasema kwa watu.

"Watoto wa kike bado wapo katika hatari kubwa sana, wanafanyiwa ukatili huu wa kingono. Wastani wa watoto 394 kubakwa kila mwezi ni mkubwa sana", alisema Wazambi. 

Ripoti hiyo ambayo imekusanywa kutoka katika vyanzo rasmi ikiwemo polisi nchini humo, inaonesha jitihada za jamii na mamlaka zinapaswa kuelekezwa katika ndoa za utotoni kwani zimeendelea kuonekana kuwa tishio dhidi ya mustakabali wa watoto.

Teenager Mütter in Tansania
Kundi la akina mama wadogo wakihudhuria semina jijini Dar es salaamPicha: DW/K. Makoye

Katika haki za wananwake, ripoti ya kituo hicho inaonesha kuwa ukiukwaji mkubwa wa haki za wananwake, ambapo wastani wa wananwake 203 wamebakwa kila mwezi kati ya kipindi Cha Januari hadi June 2018 huku matukio ya ukatili wa kimwili yanayosababisha umauti yakitajwa kuendelea kushuhuduwa.

Aidha swala la rushwa ya ngono katika sehemu za kazi limeendelea kujitokeza ambapo sekta ya habari nchini humo, imeonekana kuathirika zaidi ambapo wanawake na wasichana wameonyeshewa kidole katika utoaji wa rushwa hiyo ya ngono.

Hata hivyo ripoti hiyo imeonesha kuimarika kwa kiwango kidogo cha haki ya kuishi katika kipindi cha miezi sita ndani ya mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka uliopita 2017, huku uhuru wa kujieleza ukionekana kuendelea kuminywa hasa kufuatia kutungwa na kutumika kwa kanuni za maudhui mtandaoni.

Mwandishi: Hawa Bihoga DW Dar es Salaam
Mhariri: Iddi Ssessanga