1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Yanayojiri kwenye changamoto za Brexit

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
6 Septemba 2019

Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Uingereza leo wanajadili mkakati wa kumjibu waziri Mkuu Boris Johnson anayetaka kuitisha uchaguzi wa mapema

https://p.dw.com/p/3PA34
Brexit - Debatte im Unterhaus
Picha: picture-alliance/dpa/AP/House of Commons/J. Taylor

Johnson amesema ataindoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya  tarehe 31 mwezi Oktoba.Wakati Uingereza imo katika kizungumkuti cha Brexit, miaka mitatu baada ya kufanyika kura ya maoni, njia zilizobakia sasa ni pamoja na ama kuondoka kwenye Umoja huo bila ya mkataba au kuachana kabisa na mchakato wa Brexit.

Kiongozi wa wabunge wa chama cha Conservative Jacob Rees-Mogg amesema Wabunge wa Uingereza watapiga kura nyingine Jumatatu wiki ijayo kuamua iwapo uchaguzi wa mapema ufanyike. Hata hivyo  vyama vya upinzani ikiwa pamoja na chama kikuu cha Labour vinataka kuhakikisha kwamba uchaguzi huo  hautampa waziri mkuu Johnson mwanya wa kuweza kuiondoa Uingereza Umoja wa Ulaya bila ya mkataba ifikapo tarehe 31 mwezi Oktoba.

Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour akiwa bungeni
Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour akiwa bungeniPicha: picture-alliance/empics/House of Commons

Kiongozi wa chama hicho kikuu cha Labour Jeremy Corbyn leo anatarajiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya video na viongozi wengine wa vyama vya upinzani kujadili suala la uchaguzi wa mapema. Hapo jana  Johnson alisema atakuwa tayari kufa ndani ya korongo kuliko kwenda mjini Brussels kuomba kucheleweshwa mchakato wa Brexit. 

Wakati huo huo mahakama kuu ya Uingereza mjini London imetupilia mbali malalamiko yaliyofikishwa mbele yake kupinga hatua ya Waziri Mkuu Boris Johnson ya kusimamisha shughuli za Bunge. Hata hivyo mahakama kuu imesema uamuzi wa shauri hilo unaweza kupelekwa katika mahakama ya rufaa.

Johnson alitangaza mwishoni mwa mwezi Agosti kwamba atasimamisha shughuli za Bunge kutoka katikati ya Septemba hadi katikati ya  mwezi Oktoba, ili serikali iweze kutangaza mpango wake mpya.

Hatua hiyo ilimchochea mwanaharakati Gina Miller, ambaye aliishinda serikali juu ya suala lingine la Brexit miaka miwili iliyopita, kufungua malalamiko kwenye vyombo vya kisheria. Baadaye waziri mkuu wa zamani John Major pamoja na vyama vingine vya upinzani viliungana na bibi Miller.

Vyanzo:/RTRE/AP