Uhariri kuhusu ushindi wa Putin | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Je wapi hasa Putin anakoielekeza Urusi?

Uhariri kuhusu ushindi wa Putin

Kremlin ndiyo inayoendesha mchakato mzima wa kisiasa Urusi na hata mara hii hakuna cha kushangaza. Ndio sababu hata matokeo ya ya ushindi wa zaidi ya asilimia 70 kwa Vladmir Putin ni vigumu kuyatolea hukumu.

Ikulu ya Kremlin ndiyo inayoendesha mchakato mzima wa kisiasa nchini Urusi na hata mara hii hakuna cha kushangaza. Na ndio sababu hata matokeo ya zaidi ya asilimia 70 ya kura ambazo zinatajwa kwamba zimekwenda kwa Vladmir Putin ni vigumu kuyatolea hukumu. Lakini kilichokuwa dhahihiri ni kwamba Warusi wengi wamemchagua yeye.

Hapana shaka yoyote kwamba Putin pia ni maarufu sana miongoni mwa jamii ya Warusi pia katika wakati huu kwa sababu Ikulu ya Kremlin kwa miaka imekuwa ikizuia kwa nguvu zote kuingia kwa mwanasiasa mwingine ambaye anaweza kuvidhibiti vyombo vya habari na kujiimarisha na hatimaye kuweza kujijengea umaarufu.

Hakuna wapinzani

Na hilo sio tu shinikizo linalowakabili wanasiasa halisi wa upinzani, kwa mfano mkosoaji maarufu wa Putin anayefahamika sana Alexej Nawalny, lakini pia wale walioko kwenye mfumo wa kisiasa wa ndani wanaoonekana kuwa nguvu ya upinzani wanaomkosoa Putin binafsi. Watu kama Waziri Mkuu Medvedev. Kando na ukandamizaji unaofanyika kupitia vyombo vya usalama, vyombo vya habari vimedhibitiwa na kutumiwa kumnadi Putin kama ndiye kiongozi pekee aliyebakia na hivyo kumfanya kuwa na fursa kubwa ya kubakia katika uongozi.

GMF | Ingo Mannteufel

Ingo Mannteufel

Nchini Urusi, hakuna ushindani wa kisiasa, na kwa kuwa hakuna ushindani wa dhati wa kisiasa katika taifa hilo matokeo ya ushindi wa kishindo kikubwa hayana maana. Ushindani wa kisiasa unaofanyika ni mchezo wa kuigiza. Wale wagombea wengine walioachiwa kuingia katika kinyang'anyiro hicho ni watu waliokuwa hawana nafasi na toka mwanzo walipangwa tu kama wagombea wa kujaza idadi na kimsingi wametimiza wajibu wao.

Ili kufanikisha hilo, Ikulu ya Kremlin ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwa hali yoyote ile mipango ya kuona kwamba Vladmir Putin anaendelea kubakia madarakani. Ilitakiwa kuhakikisha kwamba Putin anashinda kwa asilimia kubwa sana ya kura ambayo ni zaidi ya asilimia 70 ili kuuondosha kabisa wasiwasi juu ya uhalali wa matokeo.

Lakini ni wapumbavu tu ndio wanaoweza kushawishika kwa matokeo hayo ya kupangwa. Na ingekuwa busara zaidi endapo wapanga mikakati wa ikulu ya Kremlin wangelitambua hilo. Na hasa kwa kuwa huko ndiko kunakofanyika mazingaombwe mengi, mizengwe na udanganyifu wa kuyaandaa matokeo hayo.

Lakini kikubwa cha kujiuliza hapa ni: je, Putin anaeipeleka wapi Urusi katika miaka ijayo? Katika ulimwengu wa nchi za Magharibi, kuna hisia ya kile kisichofikirika na kwamba inakoelekea sera ya nje ya nchi hiyo ni katika matumizi ya nguvu, kama alivyowahi kusema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg.

Kitendo cha kutumiwa sumu ya kuuwa mishipa ya fahamu inayotumika jeshini dhidi ya aliyekuwa jasusi wa Urusi, Skripal, nchini Uingereza ni hali iliyoonesha dhahiri kwamba Putin ameshajiandaa, yuko tayari hasa kuendeleza mapambano na nchi za Magharibi. Na juu ya hilo Putin katu haoneshi kuwa mtu ambaye anapanga kubadili mwelekeo wake katika kipindi chake kipya cha uongozi. Na ndio sababu ikiwa yatakuwepo mageuzi nchini Urusi yatakayofanywa na Putin, basi yategemewe tu ya kiini macho.

Mwandishi: Ingo Mannteufel/DW
Tafsiri: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com