1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa: Maadhimisho ya miaka 100 tangu kumalizika WW1

Zainab Aziz
9 Novemba 2018

Rais wa Ufaransa anatarijiwa kuwa mwenyeji wa marais Donald Trump, Vladimir Putin na viongozi wengine wa dunia mjini Paris kwa ajili ya kuadhimisha miaka 100 tangu kumalizika Vita Vikuu vya Kwanza.

https://p.dw.com/p/37yC8
"Im Westen nichts Neues"- 1. Weltkriegsoldaten mit Gasmasken
Picha: picture-alliance/Everett Collection

Rais Emmanuel Macron amedhoofika kisiasa baada ya kufanya ziara kaskazini mashariki mwa Ufaransa ambako alilazimika mara kwa mara kutega sikio lake ili kusikiliza malalamiko ya watu juu ya sera zake ambazo haziungwi mkono na wananachi wa kawaida aliotarajia kuhusiana nao vizuri.

Ziara ya siku sita alizofanya kwenye majimbo, miji na vijiji vilivyoathirika vibaya na Vita Vikuu vya Kwanza nchini Ufaransa iliamuliwa na rais huyo mwenyewe na kuzingatiwa na ofisi yake kuwa ziara isiyokuwa na kifani kutokana na muda wake na maudhui tangu enzi ya urais wa Jenerali Charles de Gaulle.

Kwa kuzitembelea sehemu ambako mapigano yalitanda na kwa kuzitembelea kumbukumbu za vita zinazoababisha majonzi makubwa, rais Macron alifikia lengo lake mojawapo ni kuonyesha jinsi askari walivyojitoa mhanga na wakati huo huo kusisitiza tahadhari juu ya mgawiko wa a barani Ulaya na kuzuka kwa siasa za kizalendo za mrengo mkali wa kulia ambazo ni hatari zinazomtia wasi wasi.

Marcon alilazimika kuzitetea sera za serikali yake juu ya nishati. Bei za juu za petroli zimegonga vichwa vya habari. Serikali yake imeongeza bei ya mafuta ili kugharimia juhudi za kupambana na uchafuzi wa mazingira lakini hatua hiyo imewakasirisha madereva na wamiliki wa malori wanaokusudia kuipinga kwa kuzuia barabara nchini Ufaransa kote wiki ijayo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture-alliance/dpa/A. Marchi

Hata hivyo, Macron ameutetea uamuzi wake kwa kueleza kwamba ni bora kuongeza kodi ya nishati badala ya kuwatoza kodi wafanyakazi, amesema watu wanaolalamika juu ya kodi za nishati ndio hao hao wanaolalamika juu ya kuchafuliwa kwa mazingira na juu ya jinsi watoto wao wanavyoathirika na mazingira machafu. 

Kuzikabili lawama juu ya kodi ya nishati na juu ya malipo ya uzeeni, halikuwa lengo la wapambe wa Macron katika ziara alizofanya katika majimbo yaliyoathirika sana kutokana na kuondoka kwa kazi za viwandani  na kutokana matitizo katika sekta ya kilimo.

Kutokana na viwango vya umasikini na ukosefu wa ajira vilivyopo juu ya wastani wa kitaifa, hali ya kutoridhika imetanda kwenye majimbo ya kaskazini mashariki mwa Ufaransa. Hali hiyo imepalilia mbolea iliyokistawisha chama cha mrengo mkali wa kulia cha Marine le Pen aliyeangushwa katika uchaguzi wa rais na Emmanuel Macron mwaka uliopita.

Hata hivyo rais Macron amesema alifurahia fursa ya kukutana na wananchi na kuzungumzi nao ana kwa ana juu ya malalamiko yao. Amesema inapasa kufafanua kwa wananchi juu ya hatua anazochukua. Lakini kauli tatanishi zinazosikika baada ya ziara kwa kiasi fulani ni makosa yake mwenyewe.

Jumatano iliyopita, Macron alizua zogo na kuwakasirisha wayahudi wa nchini Ufaransa baada ya kumzungizia vizuri aliekuwa jemadari Phillippe Petain katika Vita Vikuu vya Kwanza, jenerali ambaye baadae alishirikiana na manazi wakati wa Vita Vikuu vya Pili lakini licha ya yote hayo anatarajia  kupata faraja atakapokuwa mwenyeji wa marais Donald Trump, na Vladimir Putin  wa Urusi pamoja na viongozi wengine.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Mohammed Khelef