1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Uingereza - Ni Boris au Corbyn?

Admin.WagnerD10 Desemba 2019

Boris Johnson ameahidi kumaliza kizungumkuti cha Brexit iwapo atachaguliwa tena baadae wiki hii. Lakini ikiwa siyo Johnson basi ni Jeremy Corbyn ambaye amefanikiwa kuficha msimamo wake kuhusu suala la Brexit.

https://p.dw.com/p/3UWed
England TV-Duell | Jeremy Corbyn und Boris Johnson
Boris Johnson na Jeremy CorbynPicha: picture-alliance/AP Photo/BBC/J. Overs

Boris Johnson, meya wa zamani wa mji wa London amepunguza utani na mizaha yake iliyozoeleka wakati akijitayarisha kwa uchaguzi Alhamisi inayokuja chini ya ahadi ya kukamilisha mchakato wa Brexit haraka iwezekanavyo.

Kura za maoni ya umma zinaashria juhudi zake za kujipigia upatu kuwa kiongozi imara na mwenye mitizamo ya kutia moyo zinafanya kazi na chama chake cha Conservative kinaweza kupata wingi wa viti bungeni.

Lakini Johnson bado amesalia kuwa kiongozi anayegawa maoni, zaidi kutokanana nafasi yake wakati wa kampeni ya kura ya maoni ya Brexit mwaka 2016 ambayo ilitawaliwa na madai yaliyotiwa chumvi kuhusu Umoja wa Ulaya na kadhia ya uhamiaji.

Matamshi yake ya kuudhi ikiwemo dhidi ya mashoga na kuwafananisha wanawake wa Kiislam wanaovaa hijab kuwa sawa na masanduku ya barua yameongezeka wakati wa kampeni.

Kimsingi wapiga kura wengi wanaamini Boris ni mwanasiasa bora kuliko kiongozi wa mrengo wa kushoto Jeremy Corbyn ambaye maoni ya umma yanamtaja kuwa kiongozi wa upinzani asiye mashahuri katika kipindi cha miaka 45 iliyopita.

Tabia ya Boris ya kukosa umakini na kupungukiwa uzingatiaji wa mambo umesababisha ashutumiwe kwa kukosa uwezo wa kuwa kiongozi thabiti.

Awaziba midomo wakosoaji wake

BdTD Boris Johnson Goal Keeper
Picha: Reuters/T. Melville

Akiwa Wazri Mkuu, Johnson amewaziba midomo wapinzani wake kwa kufanikiwa kuufanyia mabadiliko mkataba wa Brexit wa mtangulizi wake Theresa May.

''Wale ambao hawakumchukulia kuwa mtu makini walifanya makosa'' alisema Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pindi Johnson alipoufanikisha mkataba wa Brexit.

Juhudi zake zilikatishwa na uamuzi wa bunge wa kupitisha sheria ya kumzuia kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bila mkataba na kusababisha kurefushwa kwa muda wa mchakato huo hadi Januari mwaka unaokuja.

Hivi sasa anatumai ikiwa atashinda wingi wa viti bungeni anaweza kufanikiwa kupitisha makubaliano yake na Umoja wa Ulaya kabla ya muda wa mwisho wa Januri 31 kufikiwa.

Harakati za kisiasa za Johnson zimekuwa na kishindo wakati wote na hivi sasa amewekeza nguvu zote katika uchaguzi wa Desemba 12.

Ushindi wake utaacha alama muhimu miongoni mwa viongozi wenye ushawishi nchini Uingereza ikiwemo shujaa wake waziri mkuu wa zama ni Winston Churchill.

Lakini kushindwa kwake kutauweka mchakato wa Brexit kwenye mkwamo kwa sababu Corbyn na chama cha Labor bado hawajatoa dira kamili ya hatma ya Brexit.

Jeremy Corbyn: Waziri Mkuu mbadala?

Kiongozi wa upinzani Corbyn anapendekeza Uingereza ichague katika ya mkataba wa Brexit uliojadiliwa upya, kujitoa kwa sehemu tu kutoka Umoja wa Ulaya au kusalia kwenye umoja huo.

UK Vorstellung Wahlprogramm der Labour-Partei
Picha: Reuters/P. Noble

Ilani ya chama chake inaahidi mipango mizito ya kuandika upya kanuni za uchumi, kutaifisha mamalaka za nishati na amaji na kuwekeza fedha zaidi kwenye huduma za jamii.

Nguvu kubwa ya kampeni ya Corbyn kwenye uchaguzi huu haijajikita kwenye suala la Brexit, bali ahadi ya kubadili jamii ya Waingereza.

Karata muhimu imekuwa ni tuhuma dhidi ya Waziri Mkuu Johnson kuwa ana mipango ya siri ya kuubinafsisha mpango wa taifa wa afya kwa wote NHS kwenye maktaba wa kibaishara an Marekani baada ya Brexit.

Kampeni yake imeandamwa na madai ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi ndani ya chama cha Labor chini ya uongozi wake.

Licha ya ukosoaji na maoni ya umma kuonesha mvuto wake kwa wapiga kura ni wa kiwango cha chini, Corbyn ana matumaini ya kufanya miujiza uchaguzi ujao kama ilivyotokea wakati wa uchaguzi wa mapema mwaka 2017.

Wakati huo kura za maoni zilionesha chama chake kikiwa nyuma kwa alama 20 dhidi ya Conservative.

Lakini msisimko ulotokana na hotuba zake kwenye kampeni ulikiwezesha chama chake kupata asilimia 40 ya kura kikiwa nyuma ya Conservative kwa asilimi 2.4 pekee.