1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai amtaka Rais Mbeki kutomkingia kifua Mugabe

Scholastica Mazula13 Februari 2008

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai amemtaka rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki kuonyesha msimamo thabiti na kumshinikiza Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo kuelekea katika uchaguzi mkuu :

https://p.dw.com/p/D71k
Kiongozi wa chama Kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai.Picha: AP

Akizungumza katika ziara yake mjini Johannesburg, Afrika Tsvangirai, amesema kwamba ni wakati muafaka kwa rais Mbeki kubadili msimamo wake na kuziweka kando sera zake za kutomkosoa kiongozi huyo wa Zimbabwe.

Aidha anasisitiza kwamba hivi sasa wanahitaji kuona ujasiri wa rais Mbeki, wa kusitisha msimamo wake huo wa kumuunga mkozo kiongozi ambaye amemfananisha na dikteta.

Kiongozi huyo wa chama cha Movement for Democratic change-MDC; anasema pia kwamba ni wakati sasa wa Mbeki kupaza sauti yake kwa ajili ya watu wanaohitaji uhuru na uchaguzi huru nchini humo.

Tsvangirai, anasisitiza kwamba, anaamini kabisa kuwa Mbeki ataweza kufanikiwa yote hayo kwa sababu hawezi kupatwa na masahibu kama ambvyo wao wamekuwa wakifanyiwa.

Anafafanua kwamba hataweza kukamatwa na polisi, kufyatuliwa mabomu ya machozi, kupigwa, kushitakiwa na wala kuona mfuasi wake akiuawa.

Lakini nguvu anayohitaji kuwa nayo pia ni kuzungumza ukweli na kuona ni mambo gani anapaswa kukabiliana nayo.

Pamoja na kwamba uchumi wa Zimbabwe umeshuka chini kwa Afrika Kusini, Mbeki amekuwa kimya na kukataa kumpinga Mugabe ambaye anataka kuwania awamu ya sita ya urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe ishirini na tisa ya mwezi ujao.

Kiasi cha Wazimbabwe milioni tatu inaaminika kuwa wamekimbilia Afrika Kusini kwa lengo la kujitafutia ajira na kukimbia matatizo yaliyosababishwa na kuporomoka kwa uchumi kulikosababishwa na mfumko mkubwa wa bei ambao hivi sasa unafikia zaidi ya asilimia ishirini na sita.

Tsvangirai anasema kwamba lengola Mbeki lilikuwa ni kumshinikiza Mugabe mwenye umri wa miaka 83 ili kuzuia ongezeko la wimbi la wakimbizi ambao wamekuwa wakikimbilia Afrika Kusini.

Kwa upande mwingine, wakati joto la kampeni za uchaguzi ujao likizidi kupamba moto, Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe amemshambulia Waziri wa zamani wa fedha ambaye pia ni mgombea urais Simba Makoni kwamba amechangia pia katika kuporomoka kwa uchumi nchini zimbabwe.

Makoni aliyekuwa mfuasi wa chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF, alifukuzwa kwenye chama hicho hapo jana baada ya kutangaza kwamba anawania nafasi ya urais.Mugabe ndiye mwakilishi wa chama hicho katika uchaguzi ujao.

Wakati huohuo, Polisi wamesema kwamba watu watatu jana walimvamia Tsvangirai ofisini kwake mjini Johannesburg na kumuibia Laptop, simu na fedha kabla hawajakimbia.

Msemaji wa polisi Thembi Nkhwasu, amesema kwamba hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwa Tsvangirai pamoja na maofisa wengine wawili kutoka katika chama chake cha MDC.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2002. Tsvangira alisimama na kushutumu kwamba alishinda kwenye uchaguzi huo kwa sababu Mugabe alifanya udanganyifu wa matokeo lakini kwa sasa atasimama kidete ili kuhakikisha kwamba chama chake kinashinda.