Tsipras avuka kizingiti cha kwanza mpango wa uokozi | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Tsipras avuka kizingiti cha kwanza mpango wa uokozi

Bunge la Ugiriki limeidhinisha kwa wingi masharti magumu ya uokozi ili kuruhusu kuanza kwa majadiliano ya kupatiwa kiasi cha euro bilioni 86 za mkopo kuunusuru uchumi wa taifa hilo uliyokuwa katika kiongo za kuporomoka.

Waziri mkuu Tsipras katika mkutano wa wabunge wa Syriza.

Waziri mkuu Tsipras katika mkutano wa wabunge wa Syriza.

Mpango huo uliidhinishwa kwa kura 229 katika bunge lenye jumla ya viti 300, kukiwa na 64 waliopiga kura ya kuukata na sita waliojizuwia. Lakini waziri mkuu Tsipras aliihitaji msaada wa vyama vya upinzani vinavyoelemea Umoja wa Ulaya kupitisha hatua hizo, na kuacha alama ya kuuliza kuhusu mustakabali wa serikali yake. Tsipras alisema hakukuwa na mbadala kwa mpango huo, ambao alikiri utasababisha ugumu, lakini alisimamia uamuzi wake, akisema yeye ndiyo mtu wa mwisho kukwepa jukumu hilo

"Mimi ndiyo nitakuwa wa mwisho kukubaliana kwa hiari na mpango wa wapinzani wetu, wa mwisho kuwezesha kwa hiari yangu mpango wa kuiondoa kwenye viti hivi, serikali iliyopigana kwa moyo, kwa heshima, kwa ushupavu miezi hii yote ya majadiliano magumu," alisema Tsipras muda mfupi kabla ya kura kupigwa bungeni huku akishangiliwa.

Masharti magumu

Ili kupatiwa ufadhili wa kiasi euro bilioni 86, Ugiriki imekubali kufanya mageuzi yakiwemo mabadiliko makubwa katika mfumo wa pensheni, kuongeza kodi ya ongezeko la thamani, kufumua mfumo wake wote wa mapatano, kuchukuwa hatua kufungua uchumi na kubana matumizi ya umma.

Bunge la Ugiriki wakati likijadili juu ya makubaliano ya uokozi Jumatano usiku.

Bunge la Ugiriki wakati likijadili juu ya makubaliano ya uokozi Jumatano usiku.

Pia imekubali kutenga mali za umma zenye thamani ya euro bilioni 50 katika mfuko maalumu wa ubinafishaji ambao utakuwa kama dhamana ya makubaliano. Hatua hizo zilitajwa kama "mauaji ya halaiki ya kijamii" na spika wa bunge Zoe Constantopoulou, moja wa wabunge 38 wa Syriza walioupinga mpango huo, na kulikuwa na makabiliano ya vurugu kati ya waandamanaji na polisi nje ya bunge, wakati mjadala ukiendelea kabla ya kura.

'Niko tayari kujiuzulu'

Miongoni mwa waasi wa Syriza alikuwa waziri wa zamani wa fedha Yanis Varaoufakis, alietimuliwa na Tsipras wiki iliyopita na ambaye aliyapinga makubaliano ya uokozi na kuyaita "Mkataba mpya wa Versailles" - Mkataba uliyoitaka Ujerumani kulipa fidia isiyoweza kuzimudu baada ya kushindwa katika vita kuu vya kwanza vya dunia.

Waziri wa nishati Panagiotis Lafazanis na naibu waziri wa ajira Dimitris Stratolis pia walipigakura dhidi ya mpango huo. Wakati kukiwa na uvumi kwamba mawaziri hao wote wanaweza kupoteza ajira zao, yumkini mapema Alhamisi, Lafazanis alisema anaendelea kuwa mtiifu kwa serikali lakini yuko tayari kukabidhi barua yake ya kujiuzulu, na kujiunga na naibu waziri wa fedha Nadia Valavani aliejiuzulu mapema siku ya Jumatano.

"Ikiwa wakati wowote barua yangu ya kujiuzulu itahitajika, niko tayari kumpatia waziri mkuu. Ni haki yake na naheshimu hilo na namhusudu. Alexis Tsipras ndiyo waziri mkuu wa nchi hii kutokana na matakwa ya Wagiriki. Tunamuunga mkono, tunaiunga mkono serikali, na hata baadhi miongoni mwetu waliopiga kura ya hapana tunaunga mkono juhudi ka kuondoka katika mgogoro huu, alisema Lafazanis.

Abadili msimamo

Tsipras aliechaguliwa mwezi Januari mwaka huu kwa ahadi ya kufuta masharti ya kubana matumizi, alibadili msimamo kufuatia majadiliano magumu ya usiku kucha mjini Brussels siku ya Jumatatu, akisalimu amri kwa matakwa ya wakopeshaji ili nchi yake ipatiwe fedha za haraka kuepusha uondokaji ambao ungesababisha machafuko katika kanda ya sarafu ya pamoja.

Waandamanaji wakikabiliana vikali na polisi nje ya jengo la bunge wakati mjadala ukiendelea.

Waandamanaji wakikabiliana vikali na polisi nje ya jengo la bunge wakati mjadala ukiendelea.

Kufuatia uidhinishaji wa bunge la Ugiriki, sasa kinachofuata ni kwa mabunge ya mataifa kuidhinisha uanzishwaji wa majadiliano na kutolewa kwa fedha ili kuziwezesha benki za Ugiriki kufungua tena, zaidi ya wiki mbili tangu serikali ilipoweka marufuku ya kuhamisha fedha nje ili kuepusha mfumo wa benki kuporomoka.

Wakati ambapo Ugiriki inakabiliwa na muda wa mwisho wa Julai 25 inapotakiwa kulipa deni la euro bilioni 3.5 kwa benki kuu ya Ulaya ECB, maafisa walikuwa wanakimbazana kuidhinisha ufadhili wa muda ambao ungeisaidia Athens kuepuka kushindwa kulipa.

Fedha kutolewa EFSM

Licha ya upinzani mkali kutoka kwa Uingereza na Jamhuri ya Czech - mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yasiyotumia sarafu ya euro - mkopo wa euro bilioni 7 unatarajiwa kutolewa kwa Ugiriki kutoka mfuko wa utulivu wa kifedha barani Ulaya EFSM - ambao ni wa jumuiya nzima na usiyosghulikia mahitaji ya fedha ya kanda ya euro.

Baada ya mgogoro wake mbaya zaidi tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia, uchumi wa Ugiriki umepoteza zaidi ya robo ya pato lake na zaidi ya moja katika kila wafanyakazi wake wanne hana ajira. Haijabainika wazi ni namna itaweza kumudu mzigo wa moja ya mipango ya kubana matumizi yenye masharti magumu zaidi kuwahi kuwekewa nchi ya kanda ya euro.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: Sekione Kitojo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com