Trump na Putin wazungumza kuhusu vita na amani
10 Machi 2026
Ikulu ya Kremlin imesema Trump alimpigia simu Putin, katika mazungumzo ya kwanza kati ya viongozi hao wawili mwaka huu na wakajadili mapendekezo ya Urusi ya kumaliza kwa haraka mzozo nchini Iran, hali ya kijeshi nchini Ukraine na athari ya Venezuela kwenye soko la mafuta duniani.
Akihutubia waandishi wa habari katika klabu yake ya gofu huko Florida, Trump alisema walikuwa na mazungumzo mazuri na rais Putin katika mkutano ulioandaliwa kwa njia ya simu na kushirikisha waakilishi wa pande zote mbili.
''Tulikuwa tunazungumza kuhusu Ukraine, ambayo ni vita visivyomalizika. Na ukiangalia, kuna chuki kubwa kati ya Rais Putin na Rais Zelensky ambayo haieleweki. Lakini nadhani yalikuwa mazungumzo mazuri kuhusiana na suala hilo. Pia tulizungumza kuhusu Mashariki ya Kati. Na anataka kusaidia. Nilimwambia anaweza kusaidia zaidi kwa kumaliza vita vya Urusi nchini Ukraine. Hiyo itasaidia zaidi.''
Trump pia amesema wanaondoa vikwazo fulani vinavyohusiana na mafuta kwa baadhi ya nchi ili kupunguza bei bila ya kutaja nchi husika.
Vita vyasababisha mzozo wa nishati duniani
Mazungumzo hayo yalifanyika ndani ya masaa machache baada ya matamshi ya Putin kwamba vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimesababisha mzozo wa nishati duniani, huku akionya kuwa uzalishaji wa mafuta unaotegemea usafirishaji wa bidhaa hiyo kupitia Mlango Bahari wa Hormuz unaweza kusitishwa hivi karibuni.
Putin amesema Urusi ambayo ni nchi ya pili inayoongoza kwa mauzo ya mafuta duniani na mmiliki wa hifadhi kubwa zaidi za gesi asilia, iko tayari kushirikiana tena na wateja wa Ulaya ikiwa watataka kurudisha ushirikiano wa muda mrefu.
Wakati huo huo, mshauri wa mambo ya nje wa ikulu ya Urusi Yuri Ushakov, amesema mazungumzo na Trump yalikuwa ya tija na yenye uwezekano wa kuwa na umuhimu kwa ushirikiano zaidi kati ya nchi hizo mbili.
Kusitishwa vita Ukraine ni kwa manufaa ya Marekani
Ushakov amesema Trump anaamini kwamba kusitishwa kwa haraka kwa vita nchini Ukraine ni kwa manufaa ya Marekani.
Katika wakati ambapo kuna msukosuko kwenye soko la nishati duniani, utawala wa Trump unafikiria kupunguza vikwazo vya mafuta kwa Urusi, huku tangazo hilo likitarajiwa hivi karibuni. Haya ni kwa mujibu wa vyanzo vilivyoko karibu na mazungumzo ya mipango hiyo.
Vyanzo hivyo vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, vimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba mazungumzo hayo yanaweza kujumuisha kuondolewa kwa vikwazo vingi pamoja na chaguo la kulengwa kwa nchi fulani, kama vile India, kununua mafuta ya Urusi bila hofu ya faini za Marekani, zinazojumuisha ushuru.