Trump azionya Urusi na Korea kaskazini | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump azionya Urusi na Korea kaskazini

Katika mkesha wa mkutano wa kwanza na rais wa Urusi Vladimir Putin,rais Donald Trump ameapa kupambana na njia mpya za  uchokozi,zinayalenga mataifa ya magharibi na kutoa wito kwa Urusi kuacha kuchochea machafuko duniani.

Hata hivyo katika  mkutano  na  waandishi  habari  pamoja  na  rais  wa  Poalnd Duda alishindwa    kuishutumu  moja  kwa  moja Urusi  kwa  kuingilia uchaguzi  wa  Marekani. Sekione  Kitojo  na  taarifa  zaidi.

Akitiwa  shime  na  kundi  kubwa  lenye  hamasa  nchini Poland likiimba  jina  lake, Trump  aliamua  kuonesha  kwamba  hazifumbii macho  hatua  za  Urusi  ambazo  zimezusha  heka  heka  kubwa duniani, hususan  kutoka  kwa  mataifa  jirani  ya  mashariki  na   na eneo  la  kati  barani  Ulaya. Ameonya  kwamba  maslahi  ya  mataifa ya  magharibi  yanaingia  majaribuni  kwa  propaganda , uhalifu  wa kifedha na  vita  vya  mtandaoni," na  kuilazimisha  jumuiya  ya NATO  kujibadilisha.

Polen Rede US-Präsident Donald Trump in Warschau (Reuters/C. Barria)

Umati wa watu waliokuwa wakimshangilia Trump katika uwanja wa Krasinski mjini Warsaw

"Tunaitaka  Urusi  kusitisha  vitendo  vyake  vya  kuyumbisha  nchini Ukraine  na  kwingineko, na  kuunga  mkono  serikali  korofi  ikiwa  ni pamoja  na  Syria na  Iran, na  kujiunga  na  jumuiya  ya  mataifa yanayowajibika  katika  mapambano  yetu  na  adui  wetu  wa pamoja na  kulinda  ustaarabu wenyewe," Trump  alisema  katika hotuba  katika  eneo  la  uwanja  wa  Krasinski  mjini  Warsaw.

Trump ahoji ukweli wa vyombo vya ujasusi

Ni ukosoaji  ambao  rais  huyo  hakuonekana  kuuelekeza  kwa vitendo  vya  Urusi mwaka  jana  wakati  wa  kampeni  yake  ya urais. Katika  mkutano  na  waandishi  habari  kabla  ya  hotuba yake, Trump alihoji ukweli  wa  vyombo  vya  kijasusi  vya  Marekani juu  ya  kuingiliwa  na  mataifa  ya  kigeni  katika  uchaguzi  wa Marekani, akidai  kwamba  Urusi  haikuwa nchi  pekee  ambayo huenda  iliingilia  uchaguzi  huo. Akizungumza  katika mkutano  na waandishi  habari  pamoja  na  rais  wa  Poland Andzej Duda , Trump alisema.

Polen PK vom US-Präsident Donald Trump und polnischer Präsident Andrzej Duda (picture-alliance/PAP/R. Pietruszka)

Trump (kushoto) akiwa na rais wa Poland Andrzej Duda katika mkutano na waandishi habari

"Nadhani  ni  Urusi , na  nadhani  inawezekana  kuwa  watu  wengine katika nchi  nyingine. Inawezekana  kuwa  ni  watu  wengi  waliingilia. Nilisema  kwa urahisi  sana,  nafikiri  inaweza  kuwa  ni  Urusi, lakini nafikiri  inaweza  kuwa  mataifa  mengine na  siwezi kunyoosha kidole  moja  kwa  moja, lakini  nafikiri  watu  wengi waliingilia. Nafikiri imetokea  kwa  muda  mrefu, ilikuwa  inatokea kwa  miaka  mingi , mingi sana."

"Hakuna  mtu  kwa  kweli  anayefahamu kwa  uhakika,"  amesema Trump.

Akianza  ziara  yake  ya  pili  nje  ya  nchi  akiwa  rais, Trump pia aliionya  Korea  kaskazini  kwamba  anafikiria "kufanya  vitu  fulani vizito" kujibu  hatua  ya  taifa  hilo  lililotengwa  kufanya  majaribio  ya makombora  ambayo  yana  uwezo  wa  kufika  Marekani licha  ya kwamba  alikataa  kutoa  maelezo  maalum  kuhusu  hilo. Trump aliyataka  mataifa  duniani  kote  kupambana  na  tabia  mbaya  ya Korea  kaskazini.

Russland TV Der direkte Draht zu Putin (picture-alliance/dpa/Sputnik/M. Klimentyev)

Rais Vladimir Putin

Pia  alitangaza  bila  kusita  kwamba  Marekani  inasimama  nyuma ya  kifungu  namba  5 cha  katiba  ya  NATO  kinachohitaji Marekani kuyalinda  mataifa  mengine  wanachama  iwapo moja litashambuliwa. Katika  ziara  yake  ya  kwanza  barani  Ulaya  kama rais  wa  marekani  mwezi  Mei , Trump  alikataa  kudhibitisha  hitaji hilo.

Trump na  Putin wanatarajiwa  kukutana  kesho  Ijumaa  mjini Hamburg, Ujerumani , pembezoni mwa  mkutano  wa  kilele  wa kimataifa  wa  G20.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape / afpe

Mhariri: Idd Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com