1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utamaduni

Thamani ya samani za kale za Kiswahili na uhifadhi wake

12 Juni 2026

Umeshawahi kutembea mitaani ukatafakari unayoyaona, hasa namna samani za kale za Kiswahili zinavyoendelea kutumika hadi leo, na kujiuliza kwa nini samani hizi bado zinapendwa, licha ya kuibuka kwa samani za kisasa?

https://p.dw.com/p/5FHAQ
Mombasa, Kenya 2026 | Utamaduni | Samani za kale (Viti na Meza)
Samani za kale za Kiswahili ni alama ya ustaarabu wa Waswahili Picha: Fathiya Omar/DW

Katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki, hususan Mombasa, Lamu na Zanzibar, kuna urithi mkubwa wa samani za jadi ambao umeendelea kuwavutia watu kwa vizazi vingi. Licha ya kuwa za kale, samani hizi bado zinatumika majumbani, katika hoteli za kifahari na hata kwenye maeneo mbalimbali ya biashara.

Kwa nini bado zinapendwa? Samani za jadi za Kiswahili zinajumuisha viti vilivyochongwa kwa ustadi mkubwa, vitanda vya kale maarufu kama mwakisu, makabati ya mbao ngumu pamoja na milango yenye nakshi za kuvutia.

Kwa Waswahili wa zamani, samani hizi hazikuwa za matumizi pekee. Zilikuwa alama ya hadhi, utajiri na utambulisho wa familia. Kila mchoro na pambo lilikuwa na maana maalumu iliyotokana na mila, tamaduni, dini na maisha ya jamii ya Waswahili.

Historia ya samani za kale

Najash Abdul Ahmed, mwalimu, fundi na mhandisi, anasema kuna historia nzuri sana na nafasi ya samani hizi katika jamii ya Waswahili. Kulingana na Ahmed, kando na vitanda, kulikuwa na viti tofauti tofauti, vitanda na makasha. Na hivyo vyote vinaenda kulingana na uwezo wa mtu. Kwani kila ukiwa una uwezo zaidi, utatengenezewa samani hizo kwa kutumia vifaa vya thamani kwa mfano viti vilivyoitwa vya kifalme ama viti vya sultani.

"Sasa viti vile ukiwa na uwezo zaidi zamani utatengeneza kwa kutumia mbao ya mpingo ambayo ni iron wood au ebony na ilikuwa ikitiwa zile tone zake zilizokuwa ni pembe za ndovu kwa wakati huo," alibainisha Ahmed.

Kwa mujibu wa Ahmed, hivyo kilikuwa ni kiti cha mtu mwenye uwezo, mwenye pesa na mwenye haiba. Kisha kulikuwa na viti vingine vya Kiswahili kama kiti cha Siu ambacho ni mfano wake, lakini tofauti hakikutumia vifaa kama vile vilivyotumika katika kiti cha kifalme.

Mombasa, Kenyaa 2026 | Utamaduni wa Waswahili | Samani za kale
Aina ya kiti kilichokuwa kinatumiwa na sultaniPicha: Fathiya Omar/DW

Kwa mujibu wa wataalamu wa utamaduni, ufundi huu ulianza karne nyingi zilizopita kutokana na mwingiliano wa Waswahili na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali yaliyokuwa yakifika katika pwani ya Afrika Mashariki.

Mchanganyiko huo wa tamaduni uliathiri usanifu wa nyumba na pia utengenezaji wa samani, jambo linaloonekana hadi leo katika nakshi na miundo mbalimbali ya samani za Kiswahili.

Kilichozifanya samani hizi zidumu kwa muda mrefu ni matumizi ya mbao imara pamoja na ufundi wa mikono uliokuwa ukizingatia ubora na umakini mkubwa. Baadhi ya samani zilizotengenezwa zaidi ya karne moja iliyopita bado zinatumika hadi leo.

Vijana wanaojifunza ufundi wa jadi wanapungua

Hata hivyo, urithi huu unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupungua kwa idadi ya vijana wanaojifunza ufundi huu wa jadi. Ahmad anabainisha kuwa shida kubwa ni kwamba vijana wa sasa na tangu kuanza kwa matumizi ya teknolojia, wanazikimbia kazi za mikono.

"Vijana wa sasa wanataka kufanya kazi za maofisini na kukaa katika viti na meza, ingawa teknolojia hii pia imeleta mashine zinazoitwa CNC zinazoweza kuchonga kwa kutumia programu za kompyuta. Wakati mwingine vijana wanaingia upande huo, lakini bado kuna wateja wengi wanaopendelea kazi ya mikono kuliko ile inayotengenezwa na mashine," alifafanua Ahmed.

Licha ya changamoto hizo, samani za kale za Kiswahili bado zinaendelea kuthaminiwa. Katika hoteli nyingi za pwani, majengo ya kihistoria na hata nyumba za kisasa, samani hizi hutumika kama mapambo na pia kama njia ya kuhifadhi utamaduni.

Mombasa, Kenya 2026 | Utamaduni wa Waswahili | Samani za kale
Meza yenye kioo inayotumika kwa ajili ya kuwekea mapambo ya mwanamkePicha: Fathiya Omar/DW

Wageni na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani huvutiwa na uzuri wake pamoja na kazi ya mikono iliyowekwa katika utengenezaji wake. Mmoja wa wapenzi wa samani za kale za Kiswahili Oneamus Maina, anasema kwa upande wake bado anazipenda na kuzitumia samani hizo.

"Nazipenda sana kwa sababu ni nzuri na ukinunua ukaziweka nyumbani, nyumba yako inakuwa tofauti kabisa na zile samani nyingine. Mimi napenda zaidi milango kwa sababu imechongwa vizuri, ina maua mazuri na mtindo wake ni tofauti na mingine ya kawaida," alisisitiza Maina.

Umuhimu wa kuhifadhi urithi wa kale

Aidha, samani hizi zimeendelea kuwa chanzo cha ajira kwa mafundi wanaozitengeneza na kuzikarabati huku wakiurithisha ujuzi huo kwa vizazi vipya. Kwa hakika, samani za kale za Kiswahili ni zaidi ya mbao zilizochongwa. Ni alama ya ustaarabu wa Waswahili na kumbukumbu ya historia iliyojengwa kwa vizazi vingi.

Kadri dunia inavyobadilika na mitindo mipya kuendelea kuibuka, jukumu la kuhifadhi urithi huu linaendelea kuwa muhimu ili vizazi vijavyo viweze kujifunza na kujivunia historia yao. Kwa sababu samani hizi si vifaa vya matumizi tu, bali ni utamaduni, historia hai, na urithi unaostahili kuhifadhiwa.