1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yawataka wawekezaji kujihusisha na sekta ya nishati

11 Juni 2024

Serikali ya Tanzania imezitaka taasisi za kimataifa kuwekeza katika sekta ya nishati ikihoji kwamba licha ya changamoto ya umeme, taifa hilo la Afrika Mashariki lina mazingira rafiki kwa uwekezaji.

https://p.dw.com/p/4gvJo
Tanzania yahitaji kuboresha uzalishaji wake wa umeme
Tanzania yahitaji kuboresha uzalishaji wake wa umemePicha: Ahmed Jallanzo/epa/picture alliance

 Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania  Dotto Biteko alishiriki mjini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa nishati uliolenga kupata suluhisho la changamoto za nishati Afrika, sambamba na kubadilishana uzoefu katika sekta ya nishati.

Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati alitumia fursa hiyo kuzisihi kampuni za wazawa na za nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya nishati, na akazitaja sababu zinazoifaifanya Tanzania kuwa taifa salama kwa uwekezaji.

''Ni muhimu sana kuangazia sekta ya binafsi'', alisema Biteko. 

Waziri Biteko ameishukuru serikali ya Ujerumani chini ya usimamiI wa Balozi wa Ujerumani Tanzania, Thomas Terstegen kwa kuendelea kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Biteko amesema kampuni za nje ikiwamo za Ujerumani zina nafasi kubwa ya kuwekeza Tanzania, kwani Tanzania bado inakabiliana na changamoto za kifedha, huku akibainisha fursa kwa kampuni za nje kuzijengea uwezo kampuni za nishati zinazosimamiwa na serikali na wazawa.

Wawekezaji kutoka Ujerumani

Serikali ya Tanzania yawahimiza wawekezaji kuwekeza katika sekta ya nishati
Serikali ya Tanzania yawahimiza wawekezaji kuwekeza katika sekta ya nishatiPicha: Office of the Deputy Prime Minister of Tanzania

Mwakilishi wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Ujerumani Djok Flom, amesema mkutano huu unafanyika kama sehemu ya mchakato wa serikali ya Ujerumani wa kuendeleza ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania kwenye sekta ya nishati.

Flom amesema, kuna kampuni zaidi ya 7 za Ujerumani ambazo zinadhamiria kuwekeza Tanzania na hivyo kampuni hizo zinatafuta kampuni za wazawa ili kufanya nao kazi katika sekta ya nishati mbadala, viwanda na biashara.

"Tumemsikia Waziri akisema wazi na kusisitiza kuwa Tanzania na ujerumani wana ushirikiano mkubwa kwa serikali na hata kwa sekta binafsi, tumefurahi kusikia Waziri akitilia mkazo suala la ushirikiano." alisisitiza Flom.

Brian Omega, Mkurugenzi wa kampuni ya Soveignty Afrika Mashariki yenye makao yake makuu Ujerumani, inayojishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya umeme wa jua, amesema.

''Nimekutana na wadau wengi sana wa Tanzania, katika sekta ya nishati, watunga sera, tanesco, tumeona kuwa Afrika mashariki ina fursa nyingi za kuwekeza katika nishati.", alisema Omega.

Aidha katika mkutano huo viongoi wa kampuni za nishati, walipata wasaa wa kujadili hali ya sasa ya usambazaji wa nishati ya umeme nchini Tanzania,  kujadili makali yao ya ushindani katika kuboresha matumizi ya nishati na kutumia nishati mbadala  sambamba na kubadilishana uzoefu katika teknolojia na fursa za uwekezaji Tanzania.