Tanzania yateketeza nyavu na zana haramu za uvuvi
26 Januari 2017Kitoweo cha samaki na dagaa licha ya kuwa muhimu katika ukanda wa maziwa makuu barani Afrika, uvuvi katika Ziwa Tanganyika nchini Tanzania unakabiriwa na changamoto nyingi ikiwemo urasimu wa upatikanaji wa leseni, uvuvi haramu na uelewa mdogo kuhusu shughuli za uvuvi.
Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Kigoma imefanya operesheni ya kuteketeza nyavu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 480 zilizokamatwa zilizokamatwa kaatika ziwa Tanganyika zikihusishwa na uvuvi haramu.
Akitekeleza zoezi hilo mkuu wa mkoa Meja jenerali mstaafu Emanuel Maganga amesema itapambana vikali na wavuvi haramu pamoja na waigizaji, wauzaji na watumiaji wa zana zisizoruhusiwa katika uvuvi.
Wakati huo huo serikali ya Tanzania imekanusha kuwepo kwa Uvuvi unaotumia sumu katika ziwa Tanganyika. Hivi karibuni zilisambaa taarifa kuwa katika ziwa hilo lonalotoa huduma za uvuvi katika nchi za Tanzania, Burundi na DRC kwamba sumu hutumika kuua samaki.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Meja Generali mstaafu Emmanuel Maganga ametoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari akikanusha na kufafanua kwamba samaki waliokutwa wameharibika hawakuuwawa na sumu.
Meja Jenerali maganga ameeleza kuwa kilichobainika baàda ya uchunguzi ni samaki wanaoharibika ni wanaonaswa na nyavu katika kina cha chini na kuchelewa kuvuliwa hasa nyakati za usiku ambapo maji ya ziwa huwa ya moto.
Afisa Uvuvi mkoa wa Kigoma Bi. Ritha Mlinga ameonya kuwa wavuvi wote wanaoweka mitego au nyavu na kuziacha ziwani kwa muda mrefu wanapaswa kuacha Tabia hiyo kwani kwa kufanya hivyo ndio wanaosababisha kuoza kwa samaki walionaswa na mitego yao
Wakati huo huo mtafiti mkuu wa masuala ya Uvuvi Tanzania anayesimamia tafiti katika ziwa Tanganyika Dr. Ishimael Kimerei ametahadharisha kuwa endapo shughuli za uvuvi katika ziwa hilo hazitazingatia sheria ipo hatari ya kutoweka kwa aina mbalimbali ya samaki ikiwemo Migebuka na Dagaa ambazo zinatajwa kuwa na thamani katika soko la dunia.
Aidha Imebainika kuwa baadhi ya wavuvi wa samaki na dagaa katika ziwa Tanganyika wanatumia vyandarua vya kujikinga na mbu waenezao Malaria ambavyo baadhi yake vina sumu jambo ambalo ni la hatari kwa afya za watumiaji wa maji na rasilimali za ziwa Tanganyika.
Mwandishi: Prosper Kwigize
Mhariri: Josephat Charo