1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Spika wa Afrika Kusini ajiuzulu, ajisalimisha polisi

4 Aprili 2024

Aliyekuwa spika wa bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, amejisalimisha katika kituo cha polisi mjini Pretoria, siku moja baada ya kujiuzulu wadhifa wake kutokana na tuhuma za ufisadi na kula rushwa.

https://p.dw.com/p/4eQ9W
Nosiviwe Mapisa-Nqakula.
Nosiviwe Mapisa-Nqakula, aliyekuwa spika wa bunge la Afrika Kusini.Picha: RODGER BOSCH/AFP

Hii ilikuwa hatua iliyokuwa ikisubiriwa na kufuatiliwa na wengi ndani na nje ya Afrika Kusini, tangu chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kilipofichua tuhuma za ufisadi dhidi yake.

Baada ya kujisalimisha katika kituo kidogo cha polisi cha Lyttleton kilichopo Centurion nje kidogo ya Pretoria, Mapisa-Ngakula alitarajiwa kuomba dhamana ya kuachiwa atakapofika mahakamani.

Soma zaidi: Kashfa ya rushwa yamng´oa Spika wa Bunge la Afrika Kusini

Kitendo cha spika huyo wa zamani ilipokelewa kwa hisia mchanganyiko nchini Afrika Kusini, huku wengine wakionekana kufurahishwa na hatua ya spika kufunguliwa mashitaka.

Cliford Andrew, mkaazi wa Brooklyn, aliiambia DW kwamba alikuwa amefurahishwa kuona kuwa "hakuna aliye juu ya sheria."

Hata hivyo, wengine kama Baloyi Mmpo, mkaazi wa Mamelodi, hawana matumaini ya kuona spika anakutwa na hatia licha ya kwamba ana kesi ya kujibu.

Kujiuzulu kwa Mapisa-Nqakula

Mapisa-Nqakula alijiuzulu kama spika wa bunge la Afrika Kusini siku ya Jumatano (Aprili 3), akidai kuwa alifanya hivyo ili aweze kushughulikia madai yaliyotolewa dhidi yake.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Ntsikelelo Breakfast, alisema kujiuzulu kwa spika huyo "kuna maana kubwa kisiasa."

Nosiviwe Mapisa-Nqakula
Nosiviwe Mapisa-Nqakula akiongoza kikao cha bunge kabla ya kujiuzulu uspika kutokana na mashitaka ya rushwa na ufisadi.Picha: GIANLUIGI GUERCIA/AFP/Getty Images

Soma zaidi: Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma anusurika katika ajali ya gari

Mwezi uliopita nyumba ya Mapisa-Nqakula ilivamiwa na maafisa wa upelelezi ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa rushwa, japo hawakutoa maelezo kuhusu uchunguzi huo.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa spika wa bunge, mwanasiasa huyo ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama kinachotawala cha African National Congress (ANC), aliwahi kuwa waziri wa ulinzi kutoka mwaka 2012 hadi 2021.

Ni wakati huo ndipo anapodaiwa kupokea zaidi ya randi milioni nne kutoka kwa mkandarasi wa jeshi la ulinzi kama hongo.

Imetayarishwa na Bryson Bichwa/DW Pretoria