1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani Jacob Zuma anusurika katika ajali ya gari

Sylvia Mwehozi
30 Machi 2024

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amenusurika katika ajali ya gari usiku wa kuamkia Ijumaa wakati gari lake lilipogongwa na dereva aliyekuwa amelewa.

https://p.dw.com/p/4eGtb
 Durban | Jacob Zuma
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: AP/picture alliance

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amenusurika katika ajali ya gari usiku wa kuamkia Ijumaa wakati gari lake lilipogongwa na dereva aliyekuwa amelewa. Lakini kundi lake jipya la upinzani limekishutumu chama tawala cha ANC kwa kuhusika katika tukio hilo.

Msemaji wa chama cha Zuma cha Umkhonto we Sizwe (MK) Nhlamulo Ndhlela amesema katika taarifa kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, Zuma amenusurika katika ajali mbili zinazowahusisha madereva wanaodaiwa kuwa walevi.

Ndhlela amesisitiza kuwa hili linaonekana kama jaribio la makusudi la kutaka kumuua Rais Zuma mwenye umri wa miaka 81, ambaye ni mwanasiasa mkongwe na mwenye ushawishi mkubwa aliyelazimika kuondoka madarakani mwaka 2018 kufuatia tuhuma za ufisadi.

Wakati huo huo, Tume huru ya uchaguzi ya Afrika Kusini imetangaza kuwa Rais huyo wa zamani hastahili kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Mei.