SPD yaridhia kujiunga na serikali ya mseto na CDU/CSU | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

SPD YARIDHIA

SPD yaridhia kujiunga na serikali ya mseto na CDU/CSU

Wanachama wa chama cha Social Democratic (SPD) cha Ujerumani wameridhia chama chao kujiunga kwa mara nyingine tena katika serikali ya mseto na muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU wa Kansela Angela Merkel

Taarifa hii ni kulingana na vyombo vya habari vya Ujerumani hii leo, baada ya matokeo ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta, zilizoonyesha kuwa wameridhia kwa asilimia 66 miongoni mwa wanachama wake 463,000.

Matokeo hayo ya kura yatafungua njia kwa serikali iitwayo Muungano Mkuu kati ya SPD, CDU na CSU, ambao umeongoza nchini Ujerumani tangu mwaka 2013.

Vile vile, uamuzi huu wa leo unahitimisha mkwamo wa kisiasa wa takribani miezi minne katika taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya.  

Hata hivyo, wachambuzi wanasema tayari hadhi ya SPD ilishachujuka kufuatia mivutano ya ndani kati ya viongozi na pia kati ya uongozi wa juu na tawi la vijana.

Mivutano ya ndani ndio chanzo cha hali hiyo na mivutano hiyo hiyo ndiyo iliyopelekea chama hicho kilichoundwa zaidi ya miaka 100 iliyopita kupoteza hadhi yake miongoni mwa wapiga kura.

Serikali mpya Machi 14

Viongozi wa SPD, Dieter Nietan (kushoto) na Olaf Scholz, wakizungumza na waandishi wa habari kutangaza matokeo ya kura.

Viongozi wa SPD, Dieter Nietan (kushoto) na Olaf Scholz, wakizungumza na waandishi wa habari kutangaza matokeo ya kura.

Miezi zaidi ya mitano baada ya uchaguzi mkuu, serikali mpya inatarajiwa kuundwa hatimaye tarehe 14 Machi. Katika wakati ambapo chama cha CDU kimeshatangaza majina ya mawaziri wake, CSU wanatarajiwa kufuata, SPD wanasema watatangaza majina ya mawaziri wao siku mbili tu kabla ya serikali hiyo kuundwa.

Utafiti wa maoni ya wananchi uliosimamiwa ya Infratest Dimap, na kugharamiwa na kituo cha kwanza cha televisheni cha Ujerumani, ARD, umedhihirisha zaidi ya asilimia 58 wanashuku uwezo wa SPD kuongoza serikali.

Hata hivyo, mwenyekiti mteule wa SPD, Olaf Scholz, akiwa katika makao makuu ya chama chao Willy Brandt Haus, amesema mbele ya waandishi habari mara baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, kwamba zoezi hilo la kuwauliza maoni yao wanachama wa SPD limewaunganisha wana-SPD.

SPD watakabidhiwa wizara sita muhimu ikiwa ni pamoja na wizara ya mambo ya nchi za nje, na fedha. Duru za kuaminika zinasema nusu ya mawaziri hao watakuwa wanawake.

Kansela Merkel aisifu SPD

Kansela Angela Merkel ameipongeza SPD kwa kujali maslahi ya taifa.

Kansela Angela Merkel ameipongeza SPD kwa kujali maslahi ya taifa.

Kura ya mdio ya wanachama wa SPD imepokelewa kwa furaha na vyama shirika vya CDU/CSU. Kansela Angela Merkel amesema kupitia mtandao wa Twitter anasubiri kwa hamu kubwa kuendelea kushirikiana na SPD kwa masilahi ya nchi.

Viongozi wa CDU/CSU wanasema kura ya ndio kwa serikali ya muungano wa vyama vikuu, GROKO, ni ya maana pia kwa mustakbali wa Umoja wa Ulaya.

Sifa zimesikika pia kutoka mashirika ya kiuchumi. Achim Berg, wa kampuni la DigitalVerband BITKOM anasema wakati umewadia wa kutekeleza mipango ya kueneza mfumo wa digitali  kote nchini Ujerumani hadi ifikapo mwaka 2025.


Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com