DR Kongo na M23 watia saini ufuatiliaji wa usitishaji vita
14 Oktoba 2025
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa makubaliano hayo yamefikiwa kupitia mazungumzo yanayosimamiwa na Qatar.
Hatua hii inakuja baada ya pande hizo mbili kushindwa kukamilisha mkataba wa amani kufikia tarehe ya mwisho ya Agosti 18, lakini sasa kuna matumaini mapya ya kurejesha utulivu katika eneo hilo lenye migogoro ya muda mrefu.
Msemaji wa serikali ya Congo, Patrick Muyaya, amethibitisha kutiwa saini kwa makubaliano hayo. Hata hivyo, kundi la M23 halijatoa tamko rasmi kuhusu makubaliano hayo hadi sasa.
Licha ya makubaliano kati ya DRC na Kongo, bado vita vinaendelea
Licha ya makubaliano haya, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia, akizungumza mbele ya baraza la usalama la Umoja huo, amesema kuwa licha ya mazungumzo na makubaliano, kati ya DRC na Kongo, bado vita vinaendelea.
"Ingawa juhudi hizi zote za amani za Kiafrika na kimataifa ni za kupongezwa na zina matumaini, hadi leo hazijatimiza ahadi zake: usitishaji wa mapigano uliokubaliwa hauheshimiwi. Baada ya kipindi kifupi cha utulivu, pande zinazopigana zimeimarisha nafasi zao na kuanza tena operesheni za kijeshi. Hali ya kibinadamu bado ni ya kusikitisha.”
Mwaka huu, kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda lilifanya mashambulizi ya ghafla na kuteka miji mikubwa miwili mashariki mwa Congo, hali iliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwahamisha mamia ya maelfu.
Rwanda imeendelea kukanusha kutowaunga mkono M23
Ingawa Rwanda imekanusha mara kwa mara kuhusika na M23, ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Julai ilieleza kuwa Rwanda inaongoza na kudhibiti kundi hilo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, chombo maalum kitaanzishwa kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa usitishaji wa mapigano. Chombo hicho kitajumuisha wawakilishi kutoka serikali ya Congo, kundi la M23, na nchi wanachama wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ukanda wa Maziwa Makuu.
Chombo hicho kitakuwa na jukumu la kuchunguza madai ya ukiukaji wa usitishaji wa mapigano na kinatarajiwa kukutana ndani ya siku saba baada ya kuanzishwa. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO, utashiriki kama mshiriki wa ziada na kutoa msaada wa uratibu wa vifaa.