1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia yapinga kuhusishwa mwanamfalme na mauaji ya Khashoggi

Saumu Mwasimba
20 Novemba 2018

Saudi Arabia imezipinga ripoti zinazodai kwamba CIA imesema mwanamfalme Mohammed bin Salman ndiye aliyetoa maagizo ya kuuwawa Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia nchini Uturuki

https://p.dw.com/p/38ZNz
USA UANI Gipfel 2018 Adel Bin Ahmed Al Jubeir
Picha: picture-alliance/Zumapress/M. Brochstein

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia  Adel al Jubeir amezipinga ripoti zinazosema kwamba mwandishi habari Jamal Khashoggi raia wa Saudi Arabia aliyeuwawa katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo nchini Uturuki aliuwawa kwa maagizo ya mwanamfalme Mohammed bin Salman. al Jubeir amesema ufalme wa Saudi unajua kwamba madai hayo kuhusu mwanamfalme hayana ukweli na wanayapinga kikamilifu na hawatoruhusu katu majaribio ya kuuhujumu uongozi wa taifa kwa namna yoyote na kutoka kwa mtu yoyote.

Al Jubeir pia ameongeza kusema kwamba haki katika kisa cha kuuliwa Khashoggi ni kitu cha kwanza ambacho Saudi arabia inakitaka kabla hata ya Jumuiya ya kimataifa kuishinikiza haki hiyo.Juu ya hilo waziri huyo wa mambo ya nje wa Saudi Arabia amezungumzia pia jinsi nchi yake ilivyokuwa tayari kujilinda kwa namna yoyote akisema siku zote wanapendelea kupata silaha kutoka nchi washirika wake lakini pia kwa jinsi ilivyojitolea kujilinda pamoja na watu wake inataka kupata silaha inazozihitaji kutoka sehemu yoyote ile.Kauli ya waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia iliyotokana na mahojiano yaliyotolewa leo imekuja baada ya hapo jana,mfalme Salman wa nchi hiyo kuzungumza kwa yake ya kwanza mbele ya hadhara tangu alipouwawa Khashoggi,hotuba yake ikilenga zaidi katika kujionesha kwamba nchi yake itapambana na maadui wa kanda hiyo.

''Saudi Arabia itaendelea kukabiliana na itikadi kali na ugaidi na tutasimama imara dhidi ya kundi linalojaribu kuiteka dini yetu ya kweli. Tutaendelea kubeba jukumu la uongozi na kueleta maendeleo katika ukanda huu na hivyo basi kuongeza fursa za uwekezaji kikanda na kimataifa.Ufalme wa Saudi Arabia utaendelea na juhudi zake za kumaliza migogoro katika kanda na kuyatatua masuala yake huku suala la wapalestina likipewa kipaumbele.''

Frankreich Antrittsbesuch Außenminister Heiko Maas in Paris
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Camus

Nchi za Ulaya,Ufaransa na Ujerumani zimejitokeza waziwazi jana na kusema kwamba zitaiwekea vikwazo Saudi Arabia.  Jean-Yves Le Drian waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema wanapanga kuiwekea vikwazo Saudi Arabia na juu ya hilo wanataka lazima ukweli wote uanikwe kuhusu kuuliwa Khashoggi.Saudi Arabia ni mojawapo ya mteja muhimu katika sekta ya ulinzi ya Ufaransa. Mwaka jana ilinunua silaha za thamani ya yuro bilioni 1.38 kutoka Ufaransa.Ujerumani kwa upande mwingine imewawekea vikwazo raia 18 wakisaudi kuingia nchini mwake,wote wakisadikiwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi. Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ameisifu Saudia kuwa ni mshirika mzuri kabisa wa nchi yake anashinikizwa ndani ya nchi yake na chama chake mwenyewe na hata Democrat kuichukulia hatua kali Saudi Arabia kuhusiana na mauaji ya Khashoggi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/ape/AFPE/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman