1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SADC kukutana kuhusu Msumbiji

Mohammed Khelef
7 Aprili 2021

Viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika wanatarajiwa kukutana mjini Maputo kuzungumzia mashambulizi ya kigaidi nchini Msumbuji, huku Umoja wa Mataifa ukiionya Tanzania kwa kutokuwapokea wakimbizi wanaosaka hifadhi.

https://p.dw.com/p/3rfGO
Mosambik Cabo Delgado | Flüchtlinge in Cabo Delgado nach Terror Angriff in Palma
Picha: DW

Mazungumzo hayo yaliyotarajiwa kufanyika siku ya Alkhamis (Aprili 8) kwenye mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, yangelihudhuriwa na marais wa Malawi, Tanzania, Botswana, Afrika Kusini, Zimbabwe na Msumbiji yenyewe.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC,  ambayo ndiyo iliyotowa tangazo hilo, ilisema mkutano huo "utazungumzia hatua za kuchukuwa kukabiliana na ugaidi nchini Msumbiji."

Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo ya nchi wanachama 16, alisema mashambulizi yanayofanywa huko sio tu ni kitisho kwa amani na usalama wa Msumbiji, "bali pia kwa eneo zima la kusini mwa Afrika na kwa jamii ya kimataifa."

Kwa ujumla, eneo hilo la kusini mwa Afrika lilikuwa na hali afadhali zaidi ya utulivu linapolinganishwa na maeneo mengine ya kati, magharibi na kaskazini, hadi waasi wanaojitambulisha kwa siasa kali za kidini na waliopewa jina la al-Shabaab na wenyeji, kulishambulia jimbo lenye utajiri wa mafuta na gesi la Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji.

Mamlaka nchini Msumbiji zinasema sasa jeshi lake limerejesha udhibiti wa mji huo, lakini ni baada ya makumi ya watu kuuawa, na maelfu kuukimbia mji huo unaokaliwa na wakaazi 75,000.

Mosambik Cabo Delgado | Flüchtlinge in Cabo Delgado nach Terror Angriff in Palma
Wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji.Picha: DW

Umoja wa Mataifa waionya Tanzania

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa ulisema ulikuwa umepokea taarifa za kuogofya kwamba Tanzania iliwakatalia watu zaidi ya 1,000 waliokuwa wanakimbia mashambulizi ya wanamgambo kaskazini mwa Msumbiji.

"Maafisa wa UNHCR wamepokea taarifa za kutisha kutoka wakimbizi wa ndani kwamba zaidi ya watu 1,000 waliokimbia Msumbiji na kujaribu kuingia Tanzania walikataliwa kuvuuka mpaka na kupata hifadhi." Ilisema taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne (Aprili 6) na shirika hilo la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, huku likitowa wito kwa mataifa jirani kuwaruhusu wanaoomba hifadhi kuingia kwenye nchi hizo ili kunusuru maisha yao.

Mapema, UNHCR ililiambia shirika la habari la Reuters kwamba hakuwa na uwezo wa kufikia kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji au maeneo yaliyokumbwa na mashambulizi hayo, bila ya kutowa sababu.

Hata hivyo, wafanyakazi wengine wawili wa mashirika ya misaada waliiambia Reuters kuwa Tanzania ilikuwa imeyakatalia mashirika yao kufikia eneo hilo, huku upande wa mpaka wa Msumbiji ukionekana kuwa hatari kuufikia.

Mashambulizi ya hivi karibuni yaliyodumu kwa zaidi ya wiki yalihusisha uvamizi wa mji wa Palma ulioanza tarehe 24 Machi, ambao wachambuzi wa masuala ya usalama walisema ulikuwa mkubwa na uliopangwa kwa hali ya juu zaidi tangu kuanza kwa uasi huo Oktoba 2017.