1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubio akutana na Papa Leo Vatican kujadili amani

7 Mei 2026

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amekutana na Papa Leo XIV mjini Vatican katika mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili yakijikita katika juhudi za kutafuta amani ya kudumu mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/5DRFG
Vatikan 2026 | Papa Leo XIV na Marco Rubio
Waziri wa Mambo ya Nje Marekani Marco Rubio akiwa na Papa Leo XIVPicha: Simone Risoluti/Vatican Media/REUTERS

Ziara ya kiongozi huyo Vatican ilikuwa na lengo la kupunguza mvutano uliosababishwa na mashambulizi ya maneno ya Rais Donald Trump dhidi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki. 

Rubio ambaye pia ni mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, alikutana kwanza na Papa Leo kabla ya kufanya mazungumzo na maafisa wengine waandamizi wa Vatican akiwemo mwanadiplomasia mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin. Vatican na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hazikutoa mara moja maelezo ya kina kuhusu mazungumzo hayo.

Picha zilizotolewa na Vatican zilimuonyesha Papa Leo akimsalimia Rubio katika Ikulu ya Kitume kabla ya wawili hao kuketi kwa mazungumzo rasmi. Rubio aliondoka Vatican chini ya ulinzi mkali wa usalama baada ya kukaa humo kwa saa mbili na nusu.

Mvutano kati ya Trump na Papa Leo umeendelea kuongezeka katika wiki za hivi karibuni baada ya papa huyo, ambaye ndiye Mmarekani wa kwanza kuongoza Kanisa Katoliki, kuvikosoa wazi vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran pamoja na sera kali za Marekani dhidi ya wahamiaji.

Trump amekuwa akimtuhumu Papa Leo kwa kile anachodai kuwa ni msimamo laini dhidi ya Iran na hata kudai kuwa papa huyo anaiunga mkono Iran kupata silaha za nyuklia. Kauli hiyo ilipingwa vikali na Papa Leo ambaye amesema jukumu la Kanisa ni kuhubiri amani na si vita.

Papa Leo: Tunapinga juu ya silaha za nyuklia

Papa Leo amesema Kanisa Katoliki kwa miaka mingi limekuwa likipinga silaha zote za nyuklia na kuongeza kuwa dunia inapaswa kutafuta mazungumzo badala ya kutumia nguvu za kijeshi. Kauli hizo zimeungwa mkono na viongozi mbalimbali wa Kikristo pamoja na baadhi ya washirika wa Marekani barani Ulaya.

Kardinali Pietro Parolin ambaye ni Waziri Mkuu wa Vatican amesema mashambulizi ya Trump dhidi ya papa huyo hayakuwa ya kawaida kidiplomasia lakini akasisitiza kuwa Vatican bado inaiona Marekani kuwa mshirika muhimu katika masuala ya kimataifa licha ya tofauti zilizopo.

Vatikan 2026 | Papst Leo XIV na Marco Rubio
Papa Leo XIV akiwa na Waziri wa mambo ya Nje Marekani Marco RubioPicha: Simone Risoluti/Vatican Media/REUTERS

Ziara ya Rubio mjini Rome pia inatazamwa kama juhudi za kurekebisha uhusiano kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya ambao wamekuwa wakikosoa vita dhidi ya Iran.

Rubio anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Antonio Tajani, viongozi ambao pia wamemtetea Papa Leo dhidi ya mashambulizi ya Trump.

Mbali na vita vya Iran, Rubio amesema mazungumzo yake Vatican pia yanahusu hali ya Cuba pamoja na uhuru wa dini duniani. Vatican imekuwa ikihofia kauli za Trump kuhusu uwezekano wa hatua za kijeshi dhidi ya Cuba baada ya kuondolewa madarakani kwa rais wa Venezuela Nicolás Maduro mapema mwaka huu.

Wachambuzi wa siasa nchini Italia wanasema Rubio huenda pia anajaribu kujijengea taswira ya kisiasa ndani ya chama cha Republican kuelekea uchaguzi ujao wa Marekani huku Vatican ikionekana kutaka kuendelea kuwa sauti ya mazungumzo na diplomasia katika kipindi hiki cha migogoro ya kimataifa.