1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa atoa wito wa ushirikiano Afrika Kusini

3 Juni 2024

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa wito kwa viongozi wa vyama nchini humo kufanya kazi pamoja kwa ajili ya umma wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4gYfB
Südafrika Pretoria | Cyril Ramaphosa spricht nach Wahlergebnissen
Picha: UPI Photo/IMAGO

Ramaphosa ameyasema haya baada ya chama chake cha African National Congress, ANC, kupoteza wingi wake wa miaka 30 bungeni katika uchaguzi mkuu nchini humo.

Lakini katika kile kinachoashiria msukosuko unaotarajiwa katika siku chache zijazo, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyechafuliwa na tuhuma za ufisadi Jacob Zuma, alisusia hafla ya kutangazwa kwa matokeo na chama chake kimekataa kuyatambua matokeo hayo.

Hesabu za mwisho zimeonesha kuwa chama cha ANC kimepata viti 159 kati ya jumla ya viti 400 katika bunge la nchi hiyo, kikifuatiwa na chama cha Democratic Alliance kilichopata viti 87 na uMkhonto weSizwe chake Zuma kikipata viti 58.

Kutokana na kuwa hakuna mshindi wa moja kwa moja, chama cha ANC sasa kitalazimika kutafuta uungwaji mkono wa vyama vingine ili Ramaphosa achaguliwe tena na bunge kama rais.