1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa asema vurugu zilichochewa na watu fulani

Bruce Amani
16 Julai 2021

Rais Cyril Ramaphosa amesema mashirika ya usalama yamewatambua watu kadhaa wanaoshukiwa kuchochea vurugu wiki hii nchini Afrika Kusini na kuwa serikali yake haitaruhusu machafuko na ghasia kutawala.

https://p.dw.com/p/3wZIb
Südafrika | Cyril Ramaphosa
Picha: UNTV/AP/picture alliance

Ramaphosa ameyasema hayo alipotembelea Manispaa ya Ethekwini, ambayo inajumuisha mji wa bandari wa Durban, mojawapo ya maeneo yaliyoathirika pakubwa katika wiki nzima ya uporaji ambao uliharibu mamia ya maduka na kuwauwa zaidi ya watu 100.

Ameongeza kuwa wanajeshi 25,000 watapelekwa katika maeneo yenye vurugu hivi karibuni, kutoka kwa idadi ya awali ya askari 10,000. Amesema waliochochea vurugu hizo wanasakwa na maafisa wa usalama.

Utulivu umeanza kurejea kwa sehemu katika mji mkuu wa kibiashara Johannesburg, hata ingawa maduka mengi yamefungwa na operesheni katika bandari za Durban na Richards Bay zinaimarika.