1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Rais Vladimir Putin ala kiapo cha awamu ya tano ya urais

7 Mei 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin, ameapishwa ramsi hii leo tayari kuanza rasmi awamu yake ya tano ya urais itakayoambatana na mamlaka makubwa zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa baada ya kushinda uchaguzi wa mwezi Machi.

https://p.dw.com/p/4fa1x
Urusi | Rais Vladimir Putin ala kiapo cha urais
Rais Vladimir Putin wa Urusi, aapishwa kushika wadhifa huo kwa awamu ya tano Picha: Kremlin.ru via REUTERS

Kwenye shughuli ya uapisho, Rais Vladimir Putinamesema anayachukulia mamlaka ya urais nchini humo kama "jukumu takatifu". Akasisitiza katika Ukumbi wa Saint Andrew ambako amekula kiapo kwamba kuitumikia Urusi ni heshima kubwa, wajibu na jukumu takatifu, huku akiwarai raia wa taifa hilo kuvikabili vikwazo dhidi yao kwa kuungana pamoja.

"Nina imani kuwa tutapita katika kipindi hiki kigumu kwa heshima. Tutaimarika zaidi na bila shaka tutatekeleza mipango ya muda mrefu na miradi mikubwa inayolenga kufikia lengo la maendeleo."

Putin alishinda uchaguzi wa urais wa mwezi Machi kwa asilimia 87, ambao hata hivyo ulikosolewa na si tu waangalizi wa kimataifa bali pia watetezi wa haki na upinzani.

Soma pia:Putin aweka rekodi kwenye matokeo ya uchaguzi Urusi

Hata hivyo baadhi ya mataifa kama Marekani na ya Ulaya yamesusia shughuli hiyo kutokana na mvutano mkali uliochochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Putin asema milango iko wazi ya ushirikiano na mataifa mengine

Lakini kwenye hotuba yake ya leo Putin amesema Urusi haijaondoa uwezekano wa mazungumzo na mataifa hayo, ingawa akasisitiza kunatakiwa kuwepo na uwanja sawa na kuongeza kuwa Urusi iko tayari kushirikiana na mataifa mengine, lakini akionya kwamba mfumo wake unatakiwa kuwa imara dhidi ya vitisho na changamoto zozote.

Urusi | Rais Vladimir Putin aapishwa
Wageni wakiwa wanasubiri Rais wa Urusi Vladimir Putin kuingia kwenye ukumbi wa Grand Kremlin kulikofanyika sherehe za kuapishwa, mjini Moscow.Picha: Grigory Sysoyev/Sputnik Kremlin/AP/dpa/picture alliance

Soma pia: Putin asema yuko tayari kutumia silaha za Nyuklia

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema Rais Putin baada ya uapisho huenda akapendekeza waziri mkuu atakayeiongoza serikali yake ijayo, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Interfax. Kulingana na katiba yaa Urusi, serikali inatakiwa kujiuzulu wakati awamu mpya ya raia inapoanza, na kumpa nafasi rais kuteua waziri mkuu mpya bungeni. Waziri Mkuu wa sasa ni Mikhail Mishustin, ambaye pengine atateuliwa tena na Putin.

Kiongozi huyo amekuwa rais kwa karibu robo karne sasa. Anatajwa kuhudumu nafasi hiyo kwa kipindi kirefu zaidi tangu enzi ya Josef Stalin na kulingana na katiba, awamu hii mpya itafikia ukomo mwaka 2030, ambapo pia ataruhusiwa kugombea awamu nyingine ya miaka sita.

Vita vya Urusi nchini Ukraine ni jambo kubwa alilofanya katika utawala uliopita

Katikati ya utawala wake ulioanzia Urusi iliyoanza kuinukia baada ya kitisho cha anguko la kiuchumi hadi kuwa tishio la usalama wa ulimwengu na kutengwa na mataifa mengine, Putin aliivamia Ukraine na kuibua mzozo mkubwa kabisa barani Ulaya ambao haujashuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia, hatua iliyosababishwa kuwekewa msururu wa vikwazo kutoka mataifa ya Magharibi. Sasa inaigeukia China, Iran na Korea Kaskazini ili kupata uungwaji mkono.

Ukraine Odessa | Vita vya Urusi nchini Ukraine
Watu wakitazama jengo la taasisi ya elimu linalowaka moto baada ya shambulizi lililofanywa na Urusi huko Odesa nchini Ukraine, Aprili 29, 2024.Picha: Sergey Smolentsev/REUTERS

Swali lililopo sasa ni kipi hasa kiongozi huyu wa miaka 71 atafanya katika kipindi hiki cha miaka sita, si tu nyumbani kwake bali pia kwenye uga wa kimataifa. Wanajeshi wa Urusi wanazidi kuchukua udhibiti wa maeneo nchini Ukraine huku mpinzani wake Kyiv akiwa anahangaika kutokana na upungufu wa wanajeshi pamoja na silaha.

Soma pia:Zelensky asema watashinda vita dhidi ya Urusi, vita vikipindukia mwaka wa tatu

Lakini, jirani yake huyu naye hakusita kuipeleka vita katika ardhi ya Urusi kwa kuvurumisha droni na makombora na kushambulia miji ya mipakani. Na mnamo mwezi wa Februari, Putin aliapa kutimiza malengo ya Urusi nchini Ukraine na kufanya kile kinachotakiwa ambacho ni kulinda uhuru na usalama wa raia wao.

Huko nyumbani, umaarufu wa Putin unafungamana sana na kuimarisha hali ya maisha kwa Warusi wa kawaida. Alianza awamu yake ya nne mwaka 2018 kwa kuahudi kuipaisha Urusi na kuwa miongoni mwa mataifa matano yenye chumi kubwa ulimwenguni. Lakini tofauti na haya, uchumi wa Urusi umeathiriwa na vita na mamlaka zinatumia fedha nyingi mno kwenye ulinzi.

Wachambuzi wanasema kwa kuwa sasa Putin amefanikiwa kuongoza kwa awamu ya sita, serikali yake inaweza ikaanzisha hatua ambazo hazitakubalika na wengi za kuongeza kodi ili kufadhili vita na kuongeza shinikizo zaidi kwa wanaume kujiunga na jeshi.