1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Donald Trump atangaza mikakati ya mwaka 2026

18 Desemba 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amelihutubia taifa hii leo Alhamisi na kuweka wazi mipango yake ya kuifanya Marekani kuwa imara zaidi kuliko hapo awali.

https://p.dw.com/p/55Zot
Marekani Washington D.C. 2025 | Donald Trump akiwa anahutubia taifa kutokea Ikulu ya White House
Rais Donald Trump akizungumza alipolihutubia taifa kutoka katika Ikulu ya White House, Jumatano, Desemba 17, 2025, Washington.Picha: Doug Mills/The New York Times/AP Photo/picture alliance

Rais Trump alianza hotuba yake kwa kutaja orodha ndefu ya kile anachokiona kama mafanikio yake katika mwaka wake wa kwanza madarakani.

Alisema licha ya kuirithi nchi ikiwa katika hali mbaya kutoka kwa mtangulizi wake Joe Biden, lakini wamefanikiwa kuleta mabadiliko chanya kuliko rais mwingine yoyote katika historia ya Marekani.

" Wademocrat walisababisha pia kupanda kwa bei ya vyakula. Lakini tunalitatua hilo pia. Mtaona mabadiliko hayo katika pochi zenu na akaunti zenu za benki katika mwaka mpya. Baada ya miaka mingi ya mapato kushuka kwa viwango vya kihistoria, sera zetu sasa zinaongeza mshahara unaobaki mikononi mwa wafanyakazi kwa kasi ya kihistoria. Na kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, mishahara inaongezeka kwa kasi kubwa zaidi kuliko mfumuko wa bei, " alisema rais Trump.

Miongoni mwa masuala aliyoyagusia kwa kifupi ni uhalifu, uhamiaji vita dhidi ya dawa za kulevya na kuliimarisha tena jeshi la Marekani.

 

Amegusia pia suala la kupunguza bei, ambalo linaibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa Wamarekani na kuahidi taifa hilo kuimarika kiuchumi mwaka ujao katika kiwango ambacho  ulimwengu haujawahi kushuhudia.