1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar yasema Hamas iko tayari kubadilishana wafungwa

2 Februari 2024

Mashambulizi ya Israel yameuwa zaidi ya watu 100 kwenye Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia Ijumaa, ikiwa ni ndani ya masaa 24 tangu wapatanishi wa Qatar kusema kuwa Hamas ilishakubali mpango wa mabadilishano ya wafungwa.

https://p.dw.com/p/4bxLa
Msemaji wa Mambo ya Nje wa Qatar Majed Al-Ansari mjini Doha
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Qatar, Majed Al-Ansari, akitowa maelezo kwa waandishi wa habari mjini Doha.Picha: Imad Creidi/REUTERS

Wizara ya afya ya Gaza ilisema kwamba watu 105 wameuawa baina ya usiku wa Alkhamis na asubuhi ya Ijumaa (Februari 2), huku kukiwa na ripoti za uvamizi na mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Israel kwenye viunga vya mji wa Khan Younis, mji mkubwa kusini mwa Gaza na kitovu cha mashambulizi yanayoendelea sasa.

Soma zaidi: Netanyahu: Sitaridhia makubaliano ya kusitisha mapigano

Mashambulizi ya miezi inayokaribia minne yameufanya Ukanda wa Gaza kuwa "mahala pasipokalika", kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, huku mzingiro wa Israel ukipelekea upungufu mkubwa wa chakula, maji, mafuta na madawa.

Mpango wa kusitisha mapigano

Hali hiyo mbaya ya kibinaadamu na kukithiri kwa idadi ya vifo vya raia kumeifanya jamii ya kimataifa kuongeza mbinyo wa kusitishwa mapigano kwenye Ukanda huo.

Ukanda wa Gaza, Khan Younis, UNRWA
Mfanyakazi wa shirika la UNRWA akigawa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina katika mji wa Khan Younis, Ukanda wa Gaza.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar, Majed Al-Ansari, alisema siku ya Alkhamis kwamba mazungumzo ya hivi karibuni yaliyofanyika mjini Paris kati ya maafisa wa nchi yake, Marekani, Israel na Misri yamefanikisha kupatikana kwa rasimu ya mpango wa kusitisha mapigano.

Soma zaidi: Viongozi wa Kiarabu wana chaguo lipi katika mzozo wa Gaza?

“Pendekezo hilo limeridhiwa na upande wa Israel na sasa tuna ithibati ya awali kutoka upande wa Hamas pia. Tuna matumaini ya kuwa na habari njema ya kusitisha mapigano ndani ya wiki chache zijazo.“ Alisema Ansari.

Hamas yataka marekebisho

Hata hivyo, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Hamas bado haijakubaliana kikamilifu na mpango huo.

Ofisa wa Hamas Osama Hamdan
Afisa wa ngazi za juu wa Hamas, Osama HamdanPicha: Hassan Ammar/AP/picture alliance

“Hakujakuwa na makubaliano hadi sasa, sisi tunaona kuna mambo muhimu hayakuhusishwa ndani ya mpango huo. Kauli ya Qatar ni ya kukurupuka na si ya kweli.“ Chanzo kimoja kililiambia shirika hilo.

Soma zaidi: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Chanzo chengine ndani ya Hamas kilikuwa kimeiambia AFP hapo awali kwamba mpango huo wenye hatua tatu ungelianza kwa kipindi cha usitishaji mapigano cha wiki sita, ambacho ndani yake misaada zaidi ingelifikishwa ndani ya Ukanda wa Gaza kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji mkubwa.

Ndani ya kipindi hicho, wanawake, watoto na wagonjwa wanaoshikiliwa na kundi hilo wataachiliwa huru kwa mabadilishano ya wafungwa wa Kipalestina ndani ya Israel.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kutaendelea kufanyika majadiliano juu ya kuondoka moja kwa moja kwa wanajeshi wa Israel ndani ya Gaza, na pia uwezekano wa awamu nyengine za kubadilishana wafungwa baina ya pande hizo mbili.

 AFP, Reuters