1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin akutana na Bush

Maja Dreyer2 Julai 2007

Rais Putin wa Urusi, yumo nchini Marekani kwa mazungumzo na rais George W. Bush. Viongozi hao wawili wanakutana mjini Kennebunkport, Kaskazini mwa Marekani, ambapo familia ya Bush ina nyumba yake ya likizo. Lengo la mkutano huo ni kuzungumzia masuala kadhaa ya kimataifa, hasa lakini kuonyesha kwa uhusiano kati ya Marekani na Urusi si mbaya kama inavyotajwa.

https://p.dw.com/p/CHBn
Putin na Bush wakiwa Kennebunkport
Putin na Bush wakiwa KennebunkportPicha: AP

Aliyempokea katika kiwanja cha ndege na kumsindikiza hadi nyumba ya familia ya Bush mjini Kennebunkport ni rais wa zamani wa Marekani, George Bush, baba yake rais wa sasa George W. Bush. Huko Putin akakutana na rais wa sasa, wote wakivaa nguo zisizo rasmi kabisa, bila ya tai kama kuonyesha kuwa si mkutano rasmi. Lakini inasemekana kuwa ni heshima kubwa kumwalika Putin kuja Kennebunkport akiwa ni mgeni wa kwanza, kiongozi wa nchi ya kigeni, kualikwa kwenye nyumba hii ya familia ya Bush.

Kabla ya ziara hiyo kuanza, wasemaji wa Ikulu ya Marekani na vilevile wa rais Putin waliupuuza umuhimu wa mkutano huu wakisema kuwa ni mkutano wa kibinafsi. Kula pamoja na kwenda kuvua samaki kwa pamoja – yaani umuhimu wa mkutano huu hasa ni kutoa picha ya kufahamiana vizuri.

Hadi sasa hakuna taarifa rasmi. Cha pekee rais Bush alichokisema pale mbele ya waandishi wa habari alipomkaribisha rais Putin ni kusema kuwa, mkutano kwa kweli unaanza.

Leo hii, marais hao wawili wanatarajiwa kuzungumzia mivutano yao juu ya mitambo ya kufyetua maroketi ambayo Marekani inataka kuijenga Ulaya ya Kati, vilevile suala la uhuru kwa jimbo la Kosovo lililoko ndani ya Jamhuri ya Serbia na mzozo juu ya mradi wa kinyuklia wa Iran. Hapa, Bush anataka kuungwa mkono kutoka kwa rais Putin katika kuongeza vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran. Kulingana na vyombo vya habari vya Marekani kuna matumaini fulani kuwa katika suala hilo la Iran maridhiano yatapatikana.

Steven Pifer ambaye ni mtaalamu wa kisiasa wa taasisi ya uchunguzi wa wa kimataifa wa masuala ya kijeshi mjini Washington, CSIS, ana wasiwasi: “Hakuna suala lolote ambalo ninataraji suluhisho litapatikana na hivyo kuboresha uhusiano kati ya Urusi na Marekani. Kwa maoni yangu, ingewezekana kukaribiana kuhusiana na matumizi ya nishati ya nyuklia kwa njia ya amani, lakini sina uhakika ikiwa suala hilo lina uzito wa kutosha kubadilisha mwenendo wa mahusiano haya kuzidi kuwa mabaya.”

Katika miezi kadhaa iliyopita, rais Putin wa Urusi aliilaumu serikali ya Marekani kwa sera zake za kibeberu, akipinga hasa mpango wa kujenga mitambo ya kufyetua maroketi barani Ulaya. Rais Bush, kwa upande wake, aliikosoa hali ya demokrasia nchini Urusi.

Andrew Kuchins, pia wa taasisi ya CSIS, anaona sababu nyingine ya mkutano huu kufanyika: “Kwa wote wawili ni suala la jukumu lao katika historia na urithi wao. Siamini kuwa wote wawili wanataka kubeba jukumu kwa kuharibu uhusiano kati ya Urusi na Marekani.”