1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Simon Sirro Polizei Dar es Salaam Tansania
Picha: DW/S. Khamis

Polisi Tanzania: Wapinzani mlioko uhamishoni rudini nyumbani

Hawa Bihoga
19 Novemba 2020

Jeshi la polisi nchini Tanzania limewataka wanasiasa walioondoka nchini na kupata hifadhi ya makazi nje ya nchi kurejea kwani lipo tayari kuwapa ulinzi wa kutosha

https://p.dw.com/p/3lXds

Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania IGP Simon Sirro anatoa wito huo mapema leo ikiwa tayari wanasiasa wawili kutoka chama kikuuu cha upinzani chadema akiwemo aliyekuwa mgombea wa urais Tundu Lissu kuondoka nchini kwa madai kuwa usalama wake upo mashakani.Polisi Tanzania yawashikilia viongozi wa upinzani

Mkuu huyo wa jeshi la polisi amewaambia wanahabari, licha ya kuwasiliana nao na kukiandikia chama barua ya kutaka Lissu pamoja na wanasiasa wengine waliotishiwa usalama wao kuripoti ofisini kwake, wanasiasa hao hawakuonesha ushirikiano na jeshi hilo badala yake walikimbilia balozi za mataifa ya kigeni. 

Tansania Wahlen | Opposition Tundu Lissu
Mmoja wa wanasiasa anayeishi uhamishoni Tundu LissuPicha: AFP

Hali ya usalama

Aidha akielezea hali ya usalama nchini Sirro amesema, hadi sasa wanawashikilia zaidi ya watu 250 ambao wanatuhumiwa kutaka kuharibu amani kabla na baada ya uchaguzi, kwa kile alichokitaja kupitia maandamano yaliopangwa kufanyika kwa lengo la kupinga matokeo yaliomrejesha mamlakani Rais John Magufuli.

Hatimaye Lissu aondoka Tanzania

Jeshi hilo limewaambia wanahabari kuwa Katika upelelezi walikamata silaha mbalimbali ikiwemo mabomu ya kutengeneza kienyeji ambayo yalilengwa kutumika kuteketeza miundombinu kadhaa ikiwemo visima vya mafuta na tayari viongozi waliongoza vurugu hizo wametiwa nguvuni.

Katika hatua nyingine akizungumzia hali ya usalama kusini mwa Tanzania ambapo hivi karibuni kumeshuhudiwa matukio ya utekwaji, uporaji na mauaji yaliotekelezwa na makundi yanayodhaniwa kuwa yenye itikadi kali, amesema katika uchunguzi wao wamebaini kuna baadhi ya watanzania ambao wanatumika na kundi hilo la uhalifu.

Hadi sasa jeshi hilo limesema lina mawasiliano ya karibu na mataifa yote ya jirani ili kuhakikisha hali ya amani inatawala na wananchi wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kujenga taifa.