Papa kufanya ziara Uingereza | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Papa kufanya ziara Uingereza

Ziara hiyo ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita inaonekana kukabiliwa na changamoto, yakiwemo maandamano ya kuipinga.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedikto XVI.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedikto XVI.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Benedikto wa Kumi na Sita kesho anaanza ziara ya kwanza ya Kichungaji nchini Uingereza, ikiwa ni karibu miaka 30 tangu ziara kama hiyo ya Kipapa ilipofanyika. Katika ziara hiyo Baba Mtakatifu atatembelea Edinburgh, Glasgow, Birmingham na London na kukutana na kiasi Wakatoliki milioni 4.2 wa nchi hiyo. Lakini mwandishi wetu Stephen Beard anaripoti kuwa Baba Mtakatifu huenda akakabiliwa na changamoto kadhaa yakiwemo maandamano ya kuipinga ziara hiyo.

Wakati wa ziara ya kwanza ya Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki miaka 28 iliyopita, Uingereza ilikuwa na shauku ya kumuona Baba Mtakatifu. Maelfu ya watu walijitokeza kumlaki Hayati Papa Yohane Paulo wa Pili. Lakini kwa wakati huu, mrithi wake, Papa Benedikto wa Kumi na Sita hatarajii kupata mapokezi kama hayo. Terry Sanderson wa Jumuiya ya Taifa ya Kidini, ni mmoja kati ya watu wengi wanaopanga kuipinga ziara hiyo.

Sanderson alisema, ''Sisi hatupingi Ukatoliki, tunampinga Papa. Na kwa kweli tunaungwa mkono kabisa na Wakatoliki ambao pia wanashangazwa na baadhi ya mafundisho ya Papa wa sasa na ukweli ni kwamba anaonekana kulirudisha Kanisa nyuma badala ya kufikiria siku zijazo.''

Sanderson na wenzake wamejiunga na kundi linalojulikana kama 'Mpinge Papa'. Mwanaharakati wa haki za mashoga, Peter Tatchell pia ni mwanachama wa kundi hilo na anadai kuwa Wakatoliki wengi wa Uingereza wanaona makosa aliyonayo Baba Mtakatifu.

''Wakatoliki wengi, pengine idadi kubwa ya Wakatoliki wa nchi hii hawakubaliani na jinsi Papa anavyopinga matumizi ya uzazi wa mpango, mapadri wanawake, usawa kwa mashoga na matumizi ya condom ili kuzuia kuenea kwa Virusi vya Ukimwi. Katika masuala yote haya, Wakatoliki wengi wamejitoa katika njia ya Baba Mtakatifu, alisema Tatchell.''

Baadhi Wayahudi wanaopinga ziara hiyo pia watajiunga na maandamano. Wanamshutumu Papa kwa kuwa na chuki dhidi ya Wayahudi na pia wamekasirishwa na uamuzi wake wa kumuondolea kizuizi cha kutengwa katika usharika mtakatifu askofu wa Uingereza ambaye alipinga mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi. Lakini suala kubwa ni kuhusu kashfa za kuwanyanyasa kingono watoto iliyofanywa na baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki.

Changamoto nyingine itakayomkabili Baba Mtakatifu ni kuhusu ghrama zitakazotumika wakati wa ziara hiyo. Waandamanaji hao wanapinga suala kuwa wao kama walipa kodi watalipa baadhi ya gharama za Euro milioni 14 zilizotengwa kwa ajili ya ziara hiyo.

Hata hivyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Southwark, Mhashamu Peter Smith anasema amehakikishiwa kwamba hakutakuwa na matatizo yoyote.

''Hawana nia ya kuvuruga ziara hii, sio kwa upande wa kidini au kiraia. Na nadhani kwamba ziara hii itawafanya waachane na mawazo hayo. Namaanisha hakuna mtu yoyote anayeweza kuhakikisha kwamba hakutakuwa na matukio yasiyokuwa ya kawaida ambayo yanaweza kuiharibu ziara hii. Lakini hilo sio lengo, alifafanua. ''

Wakati mtazamo ukiwa katika maandamano, imekuwa rahisi kusahau kwamba kwa Wakatoliki milioni nne au zaidi, wataifurahia ziara hiyo ya Baba Mtakatifu. Kura ya maoni inaonyesha kuwa wakati robo ya watu wa Uingereza wanaifurahia ziara hiyo na asilimia kumi wanaipinga, robo-tatu hawajali lolote kuhusu ziara hiyo.

Mwandishi: Stephen Beard/ZPR/Grace Patricia Kabogo

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 15.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PCui
 • Tarehe 15.09.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PCui
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com