Obama na Netanyahu watofautiana kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama na Netanyahu watofautiana kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran

Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wana mitazamao tofauti kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran huku Obama akionya kuwa Netanyahu amekuwa na mtazamo potovu kuhusu mpango huo

Hii leo waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atalihutubia bunge la Marekani ambapo anatarajiwa kuendelea na msimamo wake kuwa mpango wa kinyuklia wa Iran ni kitisho kikubwa kwa Israel na una shahidi wa kutosha kuthibitisha hilo.

Lakini Rais Obama na maafisa wake wa masuala ya sera za kigeni hawajamuachia uwanja Netanyahu kuuponda mpango wa kinyuklia wa Iran na mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na nchi tano zenye nguvu zaidi duniani pamoja Ujerumani, kwa kusema mazungumzo hayo ya kulenga makubaliano ndiyo njia bora zaidi ya kuusuluhisha mzozo huo.

Israel na marekani zasema uhusiano ni imara

Obama na Netanyahu wote wanasisitiza kuwa uhusiano wa jadi kati ya nchi hizo mbili unasalia imara lakini rais wa Marekani ameushutumu wazi wazi msimamo hasi wa Israel dhidi ya Iran na mpango wake wa kinyuklia.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa Marekani

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa Marekani

Netanyahu amealikwa kulihutubia bunge la Marekani na spika wa bunge hilo John Boehner mwanachama wa chama cha upinzani cha Republican ambaye amekuwa akipinga sera za Obama, na Waziri mkuu huyo wa Israel na mwenyeji wake hawakuiarifu ikulu ya Rais kuhusu mualiko huo.

Netanyahu amesema hotuba yake haidhamirii kumdunisha Obama au wadhifa alio nao kwani anamheshimu sana lakini akaongeza kuwa licha ya kuwa Israel na Marekani zinakubaliana kuwa Iran haipaswa kuwa na silaha za kinyukulia, zinatofautiana kuhusu namna ya kuizuia kutengeneza silaha hizo.

Hayo yanakuja wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran Javad Zarif wakikutana Uswisi kwa mazungumzo ya siku tatu yanayotarajiwa kukamilika hapo kesho.

Saudia pia ina wasiwasi kuihusu Iran

Pia Kerry anatarajiwa kusafiri Saudi Arabia wiki hii kumhakikishia mfalme Salman kuwa makubaliano yoyote kati ya Marekani na Iran kuhusu mpango huo wa kinyuklia utazingatia maslahi ya Saudi Arabia.

John Kerry na Javad Zarif mjini Geneva kwa mazungumzo ya Iran

John Kerry na Javad Zarif mjini Geneva kwa mazungumzo ya Iran

Kuishawishi Saudi Arabia kukubali yatayofikiwa kuihusu Iran ni muhimu kwa utawala wa Rais Obama kwasababu unahitaji Saudi Arabia kushirikiana kwa karibu na Marekani kuhusu sera kadha wa kadha za kanda ya Mashariki ya kati na katika suala la masoko ya mafuta.

Mbali na Israel na wabunge wa upinzani wa Marekani, Saudi Arabia pia ina wasiwasi kuwa makubaliano yoyote na Iran kuhusu mpango wake wa kinyuklia utaipa nchi hiyo nguvu za kiuchumi na nyinginezo kutanua ufadhili wake katika makundi ya wapiganaji katika vita vya Syria, Iraq, Lebanon na Yemen.

Kwa upande mwengine, naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken amesema mzozo uliopo hivi sasa kati ya Marekani na washirika wake wa muda mrefu Israel unatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwaka ujao wakati Obama atakapomaliza muhula wake wa kuhudumu kama Rais.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com