Obama kukutana na Dalai Lama | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama kukutana na Dalai Lama

Hata hivyo hatua hiyo imepingwa na China, ambapo pia imetoa onyo kuwa mkutano kati yao huenda ukahatarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

default

Kiongozi wa dini ya Budha, Dalai Lama.

Ikulu ya Marekani-White House, imesema Rais Barack Obama bado ana mipango ya kukutana na kiongozi wa dini ya budha Dalai Lama, na kupuuzia onyo lililotolewa na China kwamba mkutano wa aina hiyo unaweza ukaathiri uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili. Serikali ya China imesema inaipinga ziara hiyo ya Dalai Lama nchini Marekani na mikutano yoyote itakayofanyika kati yake na viongozi wa Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China, Ma Zhaoxu amesema wameitaka Marekani kulitambua kwa uwazi suala la Tibet na kushughulikia masuala yote kwa umakini na ipasavyo ili kuepuka kusababisha madhara zaidi katika uhusiano wa nchi hizo mbili. Siku chache baada ya Marekani kutangaza kuiuzia Taiwan silaha zenye thamani ya dola bilioni 6.4, jana Jumanne Ikulu ya White House ilisisitiza kwamba China inapaswa kushughulikia masuala ya haki za binaadamu katika eneo la Tibet. Msemaji wa Ikulu ya White House, Bill Burton aliwaambia waandishi habari kwamba katika ziara yake nchini China mwaka uliopita, Rais Obama aliwaambia viongozi wa nchi hiyo kwamba ana mpango wa kukutana na Dalai Lama, na anakusudia kufanya hivyo.

Burton alisema Dalai Lama ni kiongozi wa kidini na kitamaduni anayeheshimika kimataifa na Rais Obama atakutana naye kulingana na hadhi yake hiyo. Katibu wa Dalai Lama amesema kiongozi huyo wa kidini anatarajiwa kufanya ziara ya siku kumi nchini Marekani baadaye mwezi huu. Mwezi Oktoba mwaka uliopita, Rais Obama alikwepa kukutana na Dalai Lama wakati alipozuru Washington. Hatua hiyo ilizusha utata, lakini Ikulu ya White House ilisema Rais Obama hakutaka kuvuruga uhusiano na China kabla ya ziara yake iliyokuwa imepangwa kufanyika mwezi mmoja baadaye. Dalai Lama ambaye alikimbilia kuishi uhamishoni nchini India mwaka 1959, anatafuta haki ya Watibet kujitawala wenyewe kutoka China, lakini serikali ya nchi hiyo imekuwa ikimtuhumu kwa kutaka utengano huo.

Marekani inazingatia kwamba Taiwan na Tibet yote mawili kama majimbo yaliyo chini ya utawala wa China, lakini wana wasi wasi kuhusu suala la haki za binaadamu kutokana na wakaazi wa Tibet wanavyotendewa. Awali China ilitangaza kusitisha ushirikiano wa kijeshi na Marekani na kutishia kuziwekea vikwazo kampuni za Marekani zilizohusika katika biashara hiyo ya silaha kwa Taiwan. Marekani nayo imeshikilia kuwa biashara hiyo haigongani na sera za nje za Marekani kuhusu China na kwamba itasaidia kuleta usalama na utulivu kwa pande zote mbili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri: M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 03.02.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LrGv
 • Tarehe 03.02.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LrGv
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com