Netanyahu yuko nchini Kenya | Matukio ya Afrika | DW | 05.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Netanyahu yuko nchini Kenya

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaendelea na kile anachokiita ziara ya kihistoria Barani Afrika, katika mpango wake wa kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiusalama na Bara hilo.

Jana Jumatatu Waziri Mkuu Netanyahu alihudhuria maadhimisho ya miaka 40, baada ya kuokolewa kwa mateka nchini Uganda, ambapo kaka yake mwenyewe aliyeongoza operesheni hiyo aliuawa.

Mchana huu, tayari Netanyahu yuko jijini Nairobi, nchini Kenya akikutana na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta. Mwenyewe Kenyatta alikuwa ziarani Israel hivi karibuni. Alipozungumza hapo jana, mjini Entebbe, Uganda, karibu na uwanja wa ndege ambapo operesheni hiyo ilifanyika, wakati mateka takriban 100 walipokuwa wakiokolewa mnamo mwaka 1976, Netanyahu amesema tukio hili linapotea taratibu na kufungua ukurasa mpya wa mahusiano ya karibu zaidi na Afrika.

"Miaka 40 iliyopita, askari wa Israel waliendesha operesheni ya kihistoria hapa Entebbe", alisema Netanyahu ambaye amekuwa waziri mkuu wa kwanza wa Israel kufanya ziara ya kwanza katika Ukanda wa Kusini mwa Bara la Afrika, baada ya miongo mingi.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Taarifa zinasema kuwa, Israel imetoa msaada wa dola za Kimarekani bilioni 13 za kuwezesha kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi za Afrika. Nchi hiyo pia inatarajia kutoa mafunzo ya namna ya kuboresha usalama wa ndani na afya.

Baada ya mkutano wa kihistoria uliokutanisha viongozi saba wa Afrika uliofanyika nchini Uganda, Netanyahu ambaye ameongozana na wafanyabiashara 80 wanaowakilisha makampuni 50 ya biashara, alielekea Kenya hivi leo, huku pia wakitarajia kuzuru Ethiopia na Rwanda.

Machafuko kati ya nchi za Kiarabu na Israel yalichangia hali ya kutengamana kati ya nchi za Afrika na mataifa ya Kiyahudi tangu miaka ya 1960. Kutokana na vita kati ya Israel na majirani zake kati ya mwaka 1967 na 1973, mataifa yaliyopo Kaskazini mwa Afrika yaliyoongozwa na Misri yalishinikiza nchi zilizopo Kusini mwa jangwa la Sahara kukata mahusiano yake na Israel, ambapo mengi yaliitikia shinikizo hilo.

Kando na mahusiano ya kidiplomasia na biashara, ziara hiyo ina maana binafsi kwa Netanyahu. Mwaka 1976, kaka yake Jonatan, aliyejulikana kwa jina la utani, "Yoni" aliuwawa wakati huo akiwa komandoo aliyeongoza mashambulizi ya ghafla mjini Entebbe nchini Uganda katika kuwaokoa abiria waliokuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Ufaransa, "Air France" iliyotekwa na Wapalestina wawili na Wajerumani wawili.

Sanamu ya Kumbukumbu ya Yonathan Netanyahu, iliyoko Entebbe, Uganda.

Sanamu ya Kumbukumbu ya Yonathan Netanyahu, iliyoko Entebbe, Uganda

"Nimejifunza kutoka kwa kaka yangu kwamba mnahitaji vitu viwili katika kukabiliana na ugaidi, uwazi na ujasiri", Netanyahu alisema. Alipozungumza katika maadhimisho hayo, alisema vita dhidi ya ugaidi vitaendelea. Alisema, iwapo magaidi wanafanikiwa eneo moja, hujisogeza na maeneo mengine, na iwapo ugaidi utadhibitiwa mahala popote, utakuwa unapunguzwa nguvu hata maeneo mengine.

Mahusiano kati ya Israel na Afrika kibiashara hivi sasa ni asilimia 2 tu, ingawa bado kunaoneka kuwepo na ongezeko la mahitaji. Lakini pia Israel inaliona Bara la Afrika kama mshirika wake muhimu, hususan ndani ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa, ambazo mara nyingi zimeitupia lawama ya kulikalia eneo la Ukingo wa Magharibi na kuweka kizuizi katika ukanda wa Gaza.

Baadhi ya nchi za Afrika zimeonyesha utayari wa kujifunza teknolojia ya kilimo na maji kutoka nchini Israel, ambazo nchi hiyo imekuwa ikizipigia debe. Ziara hii ya Netanyahu, inafuatia mikakati ya mida mrefu ya kuboresha mahusiano na Afrika.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef