1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ayakataa mapendekezo ya Hamas

Lilian Mtono
8 Februari 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekataa masharti yaliyotolewa na kundi la Hamas ili kufanikisha makubaliano mapya ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/4c9te
Israel Blinken na Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kulia), na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.Picha: GPO/Anadolu/picture alliance

Kama Israel ingeukubali mpango huo, ulikuwa ujumuishe pia kuwaachilia mateka.

Badala yake kiongozi huyo ameapa kuendelea na vita hadi “ushindi kamili utakapopatikana."

Kundi la Hamas lilipendekeza kusitishwa kwa mapigano kwa miezi minne na nusu na katika kipindi hicho mateka wote wangeachiliwa huru, Israel kuondoa majeshi yake huko Gaza na kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita.

Soma zaidi: Israel yatofautiana na Marekani kuhusu kuundwa taifa la Palestina

Netanyahu pia amepuuzilia mbali makubaliano yoyote yatakayolipa fursa kundi la Hamas kuidhibiti Gaza kwa sehemu ama kikamilifu, hali inayoashiria ukubwa wa pengo linalolisalia baina ya pande hizo mbili wakati vita vyao vikiingia mwezi wa tano.

Matamshi ya Netanyahu yanakuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akizuru ukanda huo kujaribu kuratibu makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda.