1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naibu wa Rais Kenya Ruto azuiwa kwenda Uganda

3 Agosti 2021

Uhasama kati ya Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto unaendelea kudhihirika baada ya Makamu huyo kuzuiliwa kusafiri Uganda Jumatatu jioni kwa ziara ya kibinafsi

https://p.dw.com/p/3yT0A
Kenia President Kenyatta Rede Terroranschläge 02.12.2014
Picha: AFP/Getty Images/S. Maina

Kwa mujibu wa msemaji wake, David Mugonyi, Ruto ambaye alikuwa anakwenda Uganda kwa mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja kwa kwa ziara ya kibinafsi aliambiwa na maafisa wa uhamiaji kwamba alitakiwa kupata idhini kabla ya kusafiri. 

Duru zinaelezea kuwa maafisa wa uhamiaji katika uwanja wa ndege wa Jommo Kenyatta, walisisitiza Ruto kupata kibali cha kusafiri kutoka kwa mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinywa. Hata hivyo, wasaidizi wa Ruto wamemlaumu Waziri wa Usalama wa Taifa, Fred Matiang'i, kwa kuyafanya maamuzi ya kusitisha safari ya Ruto.

Imebainika kuwa Ruto aliyekuwa anasafiri na wafanyibiashara wanne na wabunge watatu, alilazimika kukaa katika uwanja wa ndege kwa muda wa masaa matano, kabla ya kuamua kuvunja safari hiyo. Baadhi ya wabunge waliokuwa kwenye ujumbe wa Ruto ni mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, Oscar Sudi wa Kapsaret na mbunge wa Kinango Benjamin Dalu Tayari. Wabunge hao walikuwa wamezuiliwa kusafiri, lakini waliruhusiwa kusafiri baada ya mvutano wa masaa matatu. Ndindi Nyoro anafafanua. "Makamu wa rais aliwekwa hapo kwa kwa masaa matano, akisubiri kuidhinishwa, tulipoulizia ni idhini gani alikuwa akisubiri, hakuna aliyetupa jibu. Afisa wa uhamiaji alituambia amepata maagizo kutoka juu."

Fred Matiangi vorne links
Kuna mpasuko ndani ya chama tawala KenyaPicha: Imago/Xinhua Afrika

Alipokuwa ameketi kwenye ukumbi wa watu mashuhuri, Ruto alipata taarifa kuwa hakuwa na idhini ya kusafiri kwenda Uganda. Kwa mujibu wa msemaji wake David Mugonyi, Ruto alijaribu kuwasiliana kwa njia ya simu na mkuu wa utumishi wa umma, Joseph Kinywa, ambaye alisema hakuwa na taarifa kuhusu maagizo hayo. Kwenye mtandao wake wa Twitter, Ruto aliandika na ni namnukuu "ni sawa tumwachie MUNGU". Chekai Musa ni mchambuzi wa masuala ya siasa anahofia mustakabali wa siasa za nchi.

"Ni wazi kuwa Rais Kenyatta ameonyesha ukweli wake, kuwa hayuko tayari kumkabidhi naibu wake mamlaka katika uchaguzi mkuu ujao. Hili ni suala ambalo huenda likaleta msukosuko na mvutano katika uchaguzi ujao.”

Ofisi ya Waziri Matiang'i haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na masaibu ya Ruto.

Utaratibu wa Usalama wa Safari za watumishi wakuu wa umma za taifa, unasema kuwa safari za nje za makamu wa rais zinastahili kuidhinishwa na rais. Hata hivyo, safari za mawaziri na makatibu wakuu, huidhinishwa na mkuu wa utumishi wa umma. 

Hadi tukienda hewani, maandamano ya amani yalikuwa yanapangwa kufanyika katika bustani ya Freedom Corner jijini Nairobi ya kupinga hatua ya serikali ya kuzuia safari ya makamu wa rais.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi