1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mwili wa Alexei Navalny wazikwa Moscow

Saleh Mwanamilongo
1 Machi 2024

Maelfu kadhaa ya wafuasi wa mpinzani wa Urusi Alexeï Navalny walikusanyika leo Ijumaa ili kumpa heshima ya mwisho nje ya kanisa moja huko Moscow kabla ya mazishi yake, licha ya vitisho vya kukamatwa.

https://p.dw.com/p/4d5bT
Navalny amezikwa kwenye makaburi ya kusini mashariki mwa Moscow
Navalny amezikwa kwenye makaburi ya kusini mashariki mwa MoscowPicha: Olga Maltseva/AFP/Getty Images

Gari la kubeba maiti lililokuwa limebeba jeneza la mpinzani mkuu wa Vladimir Putin liliwasili mwendo wa saa saba na dakika hamsini mchana wa leo Ijumaa mbele ya kanisa, na kushangiliwa na umati wa wafuasi wake, wengine wakiimba na kutukuza jina lake.

Mlolongo mrefu wa watu, chini ya uangalizi wa karibu wa polisi, ulikuwa umeundwa tangu asubuhi mbele ya kanisa la Maria mama wa Mungu, katika wilaya ya Marino, kusini mashariki mwa jiji la Moscow, ambako Navalny aliishi alipokuwa huru. Wafausi hao ni kutoka Moscow bila shaka, lakini pia kutoka kote nchini Urusi.

''Sote tunaogopa kuja''

Wengi waliohudhuriamazishi hayo walielezea hofu na wasiwasi wa kukamatwa, mfano wa Kamilla alikuja toka asubuhi kwenye kanisa la Maria mama wa Mungu.

''Tunaogopa, sote tunaogopa kuja. Lakini tulifanya maamuzi haya katika dhamiri na woga. Navalny ndiye aliyetupa tumaini, ndiye aliyetuweka huru. Kusema ukweli inapendeza sana mimi kuwa hapa kwenye kundi la watu wenye nia moja.'', alisema Kamilla.

Ibada ya wafu ilifuatiwa na mazishi katika makaburi ya Borisovskoye, ambako wazazi wa Navalny pia waluhudhuria na kushangiliwa na umati wa waombolezaji. Makumi ya maafisa wa usalama walitumwa katika eneo hilo. Mamlaka pia walitenga eneo hilo kwenye njia inayotoka kanisani kuelekea makaburini kwa kutumia vizuizi vya chuma.

Vitisho vya Kremlin

Umati wa watu wahudhuria ibada ya kumuaga Navalny jijini Moscow
Umati wa watu wahudhuria ibada ya kumuaga Navalny jijini MoscowPicha: REUTERS

Ndani ya kanisa hilo, mashahidi kadhaa waliripoti matangazo yanayoeleza kuwa kurekodi sauti na picha ni marufuku katika eneo la kanisa hilo. Mabalozi wa Marekani, Ufaransa na Ujerumani walionekana pia kanisani, pamoja na baadhi ya wapinzani ambao bado wako huru nchini humo akiwemo Evgeni Roïzman, Boris Nadezhdine na Ekaterina Dountsova. Kulingana na imani ya Orthodox, jeneza liliachwa wazi kwa wapendwa wa Navalny kabla ya kuzikwa.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alionya juu ya uwezekano wa vikwazo kwa kushiriki katika maandamano yoyote "yasiyoidhinishwa" wakati wa mazishi. Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari wa kila siku, Dmitri Peskov pia alithibitisha kwamba hana ujumbe wowote kwa familia ya Navalny.

Heshima za mwisho za mkewe

Yulia Navalnaya, mjane wa marehemu Navalny, alitoa heshima kwa mumewe kupitia mtandao wake wa X muda mfupi baada ya mazishi yake. Navalnaya alimshukuru mumewe kwa miaka 26 ya maisha ya furaha kabisa. Navalnaya, ambaye yuko nje ya Urusi, hakuhudhuria ibada ya mazishi, aliandika ni memnukuu "Sijui jinsi ya kuishi bila wewe'', mwisho wa kumnukuu.

Navalny aliongoza wimbi la maandamano mwaka 2011-2012 ambapo alitangaza kuwa anaweza kuchukua ikulu ya Kremlin. Amefariki akiwa na umri wa miaka 47.