1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa AU Macky Sall aelekea Urusi

Saumu Mwasimba
2 Juni 2022

Rais Macky Sall atazamia kumshawishi rais Putin kufungua nafasi ya kusafirishwa chakula na mbolea ili kulisaidia bara la Afrika liondokane na madhila ya kupanda kwa bei ya bidhaa

https://p.dw.com/p/4CBB6
Macky Sall, Präsident der Republik Senegal
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni rais wa Senegal anaelekea Urusi ambako amepangiwa kesho Ijumaa kukutana na rais Vladmir Putin. Ziara hiyo inalenga kutafuta namna ya kumshawishi rais Putin kufungua njia ya kusafirishwa nafaka na mbolea

Vita vya Ukraine vimesababisha hali ya kuzuiwa usafirishaji wa bidhaa hizo na bara la Afrika hususan limeathirika kutokana na hali hiyo.

DW Premium Thumbnail | Ugandans can't buy bread because of the war in Ukraine
Picha: DW

Ukraine na Urusi zote mbili ni wafirishaji wakubwa wa ngano na nafaka nyingine barani Afrika wakati Urusi ikiwa mzalishaji mkubwa wa mbolea.

Kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Senegal ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Macky Sall kesho ijumaa kwa hivyo atakutana na rais Vladmir Putin mjini Sochi kujaribu kumshawishi rais huyo wa Urusi kupunguza mgogoro nchini Ukraine lakini pia kutoa nafasi ya kuachiwa usafirishaji shehena za nafaka na mbolea.

Ukraine-Krieg I  Kreml I  Wladimir Putin
Picha: Mikhail Metzel/Sputnik/AP/picture alliance

Na ziara hiyo imeandaliwa baada ya rais Putin kumualika rais huyo wa Senegal ambaye anakwenda Sochi pamoja na rais wa tume ya Umoja wa Afrika Musa Faki Mahammat. Aidha Umoja huo wa Afrika pia utahutubiwa kupitia kanda ya video na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ingawa bado tarehe haijatangazwa.

Vita vya Ukraine vimesababisha kupanda kwa gharama ya mafuta, nafaka na mbolea duniani na bara la Afrika limeathirika zaidi. Mwezi uliopita Umoja wa Mataifa ulisema bara hilo linakabiliwa na mgogoro ambao haukutarajiwa uliosababishwa na vita katika wakati ambapo toka hapo bara hilo linakabiliwa na matatizo yanayosababishwa kuanzia na mabadiliko ya tabia nchi mpaka janga la Corona.

Kiongozi wa Umoja wa Afrika Macky Sall mwanzoni kabisa mwa wiki hii alitowa mwito kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kusaidia kutafuta namna ya kupunguza matatizo yaliyopo kuhusu upatikanaji wa bidhaa muhimu. Kiongozi huyo alitanabahisha kwamba uamuzi wa kuyaondowa mabenki ya Urusi katika mfumo wa malipo wa kimataifa-SWIFT ni hatua inayoweza kusababisha matatizo makubwa katika usambazaji wa chakula barani Afrika.

Senegal Besuch Kanzler Scholz | Präsident Macky Sall
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Na kupitia hotuba yake kwa njia ya video kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya aliwasisitizia kwamba suala hilo liangaliwe upya na mawaziri ili kupata suluhisho mwafaka. Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika kadhalika alikiri kwamba hatua ya Urusi ya kuifunga bandari ya Odessa imeathiri shughuli za Ukraine za usafirishaji chakula na akaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kuikomboa bandari hiyo.

Ikumbukwe kwamba Urusi inakabiliwa na vikwazo chungunzima vilivyowekwa na nchi za Magharibi baada ya uvamizi wake Ukraine Februari 24, vikwazo vilivyolenga kuiadhibu Urusi.