Mvua kubwa yaendelea kuipiga Afrika Kusini | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 17.04.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Mvua kubwa yaendelea kuipiga Afrika Kusini

Mvua kubwa inaendelea kunyesha mashariki mwa Afrika Kusini eneo ambalo tayari mafuriko ya kutisha yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 400 na kuwaacha mamia kwa maelfu wengine bila makaazi.

Mafuriko yalivamia sehemu za kusini mashariki kwa mji pwani wa Durgan mapema wiki hii na kuharibu barabara, hospitali na kusomba majengo na wote waliokuwemo ndani.

Hadi sasa mafuriko hayo yameharibu nyumba 13,500, kiasi hospitali na kliniki 58 pamoja na mifumo mingine ya mawasiliano, usambazaji wa maji, nishati na barabara.

Vikosi vya uokozi viliwekwa katika hali ya juu ya tahadhari jana Jumamosi (Aprili 16) huku juhudi za kusambaza msaada wa kiutu zikiendelea katika jimbo la KwaZulu Natal kunakoshuhudiwa uharibifu mkubwa uliotokana na mafuriko.

Serikali imesema hadi sasa karibu watu 400 wamekufa na wengine 27 hawajulikani waliko. "Kwa bahati mbaya bado kuna miili inaopolewa kutoka kwenye mabaki ya majengo, hususani maeneo ya vijijini," alisema Shawn Herbst kutoka shirika la msaada wa dharura la Netcare 911.

Uharibifu mkubwa bado unashuhudiwa KwaZulu-Natal 

Mvua zinazoendelea kunyesha zinaendelea kuharibu mali na kugharimu maisha ya watu.

Afisa wa idara ya Hali ya Hewa nchini Afrika Kusini, Puseletso Mofokeng, alisema ingawa mvua za mwishoni mwa juma hazitakuwa kubwa kama iliyoshuhudiwa mwanzoni mwa wiki hii, hali ya uchepechepe kwenye udongo inaongeza uwezekano wa kutokea mafuriko zaidi.

Hata hivyo, licha ya mvua inayoendelea kunyesha mjini Durban, ligi ya kandanda ya eneo hilo imeendelea kwa kuzikutanisha timu mbili AmaZulu na Maritzburg United katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Moses Mabhida.

Lakini mechi ya mchezo wa Raga ya kuwania kikombe cha Currie kati ya wenyeji wa mji wa Durban, The Sharks, dhidi ya The Bulls kutoka mjini Pretoria iliyopangwa kutimua vumbi siku ya Jumamosi ilifutwa kuonesha heshima kwa wahanga wa janga hilo la asili.

Juhudi za uokozi zatatizwa na mvua inayoendelea kunyesha 

Vikosi vya jeshi la taifa, polisi na makundi mengi ya watu wa kujitolea ndivyo kwa pamoja vinavyoongoza operesheni ya kutafuta na kuwaokoa watu.

Wakaazi wengi wa kitongoji cha Marianhill wanaosubiri kwa shauku habari za wapendwa wao walishusha pumzi baada ya kuwasili kwa vikosi vya uokozi lakini ghafla mvua kubwa ikaanza tena kunyesha.

"Hivi sasa waokoaji wamefika, lakini kwa kuona mvua inakuja tena, watatatizika," alisema Dumisani Kanyile alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Vikosi hivyo vya uokozi vimeshindwa kumpata hata jamaa mmoja wa familia ya watu 10 ambao hadi sasa hawajulikani waliko.

Siku sita tangu mafuriko yalipolikumba eneo hilo la kwa mara ya kwanza, matumaini ya kuwapata manusura yanazidi kuyoyoma na mamlaka za mji wa Durban zimesema kwa sasa zinawekeza nguvu ya kutoa msaada kiutu na kurejea kwa maisha ya kawaida.