Murdochs kuhojiwa leo na bunge | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.07.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Murdochs kuhojiwa leo na bunge

Mmiliki wa kampuni la vyombo vya habari Rupert Murdoch, na mwanawe James Murdoch pamoja na aliyekuwa msaidizi mkuu Rebekah Brooks watahojiwa leo na kamati ya bunge kuhusiana na kashfa ya kunasa mazungumzo ya simu.

default

Mkuu wa kampuni la vyombo vya habari News International ,Rupert Murdoch, atahojiwa leo na wabunge wa Uingereza.

Mmiliki wa kampuni la vyombo vya habari Rupert Murdoch, mwanawe James Murdoch na aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni la News International nchini Uingereza, Rebekah Brooks, hii leo wanatarajiwa kufika mbele ya kamati ya bunge nchini humo kuhusiana na kashfa ya unasaji mazungumzo ya simu ilioitikisa nchi hiyo. Haya yanajiri wakati waziri mkuu David Cameron anatarajiwa kurudi leo nchini humo baada ya kukatiza ziara yake barani Afrika kushughulikia kashfa hiyo kuu.

►Rupert Murdoch, mwanawe, na Rebekah Brooks wanakabiliwa na wakati mgumu hii leo mbele ya kamati ya wanachama tofauti, ya utamaduni, uandishi habari na michezo, inayotarajiwa kuwataka watatu hao kutoa ushahidi wao kuhusu kashfa hiyo iliyoikumba kampuni hiyo kuu ya uandishi nchini Uingereza.

Alipowasili mbele ya kamati hiyo mnamo mwaka 2003, Brooks alikiri kuwa polisi ililipwa kutoa habari, lakini baadae akajisahihisha na kusema alimaanisha na sekta nzima kwa jumla ya uandishi.

Rebekah Brooks

Rebekah Brooks, mtendaji mkuu wa kampuni la News International

Bunge limewataka watatu hao wafike mbele yake baada ya Rupert Murdoch na mwanawe James, kudai kuwa hawataweza kufika. Naibu kamishna wa polisi, John Yates, aliyekataa kuanzisha uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo ambayo sasa imefungwa,mnamo mwaka 2009, alijiuzulu hapo jana baada ya mkuu wake, Paul Stephenson kuondoka pia.

Wiki iliyopita Yates alikiri kujuta kwake dhidi ya uamuzi wake huo wa awali lakini alitupa lawama zote kwa kampuni hiyo ya Murdoch kwa kushindwa kutoa ushirikiano.

Alijiuzulu alipotambua kuwa anakaribia kusimamishwa kazi.

Wakati kashfa hiyo ikiendelea kugonga vichwa vya habari, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amekatiza ziara yake barani Afrika, na anatarajiwa kurudi Uingereza hii leo jioni kuishughulikia kashfa hiyo. Katika mkutano na waandishi habari akiwa na rais wa Afrika kusini Jacob Zuma, kwa mara nyengine tena alilazimika kujibu maswali kuhusu uhusiano wake na mhariri wa kampuni hiyo ya News of The World, Andy Coulson. Cameron alisema:

'Hakuna aliyelalamika kuwa kazi aliyoifanya akiwa serikalini, kwa njia yoyote ilikuwa na makosa au ilikuwa mbaya, alifanya kazi vizuri serikalini, na baadae aliondoka serikalini'.

Coulson alijiuzulu mnamo mwezi Januari na alikamatwa tarehe 8 mwezi huu.

Awali kiongozi wa upinzani nchini humo, Ed Miliband, alizidisha shinikizo kwa waziri mkuu Cameron akimtaka aombe msamaha kwa hatua yake ya kumuajiri Coulson.

Mapema hapo jana Cameron, alitoa wito wa kufanyika kikao cha dharura bungeni, kutetea uamuzi wake wa kumuajiri mfanyakazi huyo wa zamani wa kampuni hiyo ya News of the World, kuwa mkuu wake wa kitengo cha habari.

Großbritannien Abhörskandal David Cameron in Wales

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron

Ama kwengineko katika taarifa zilizowashutusha wengi kuhusu kashfa hiyo inayoendelea, aliyekuwa mwandishi wa gazeti la News of the World, Sean Hoare, amepatikana amefariki nyumbani mwake.

Hoare ndiye aliyeliambia gazeti la New York Times kuwa unasaji mazungumzo ya simu katika gazeti hilo ulikuwa mkubwa zaidi ya ilivyokiri gazeti hilo wakati huo.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/afpe

Mhariri: Sekione Kitojo.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com