1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa chakula waingia taratibu Gaza

14 Machi 2024

Boti ya msaada wa chakula yaelekea Gaza wakati Wapalestina waliokata tamaa katika Gaza City wakisubiri kuwasili kwa msaada huo.

https://p.dw.com/p/4dV7o
Boti ya Open Arms ikiwa katika bandari ya  Larnaca Cyprus
Boti ya Open Arms ikiwa na msaada wa chakulaPicha: AFP

Msaada wa kibinadamu unaendelea kuingia taratibu katika Ukanda wa Gaza,ambapo leo boti ya kwanza iliyosheheni tani 200 za chakula ilikuwa inaelekea taratibu katika Ukanda huo huku juhudi zikiongezeka za kupelekwa msaada zaidi wa kibinadamu katika eneo hilo la Wapalestina linalozingirwa na Israel.

Shirika kubwa la msaada la Umoja wa Mataifa lililoko Gaza,UNRWA limesema Israel jana Jumatano ilishambulia maghala yake ya chakula katika mji wa Kusini wa Rafah na mfanyakazi wake mmoja aliuwawa,baadae jioni  lakini Israel ikatoa tamko ikisema imemuuwa kamanda wa kundi la Hamas,Mohammed Abu Hasna kwenye shambulio lake la roketi dhidi ya kituo cha kusambaza chakula  cha Umoja wa Mataifa.

Maafisa wa afya wa Palestina wakaripoti kwamba watu wengine wanne zaidi ikiwemo mfanyakazi wa umoja wa Mataifa waliuwawa.Soma pia: Wapalestina kadhaa wauwawa machafuko ya Ukingo wa Magharibi

Pamoja na hayo mataifa wafadhili,mashirika ya msaada pamoja na yale ya hisani wamekuwa wakiendeleza juhudi za kupeleka msaada katika Ukanda huo wa Gaza unaokaliwa na watu milioni 2.4 na ambako baa la njaa linanyemelea baada ya zaidi ya miezi mitano ya vita.

Mpaka sasa hatua za kudondosha msaada kwa ndege  pamoja na juhudi za kufunguliwa njia ya baharini zimeonesha sio mbadala wa usafirishaji wa msaada huo wa kiutu kupitia njia ya barabara,kwasababu ni sehemu ndogo tu ya msaada inayoweza kudondoshwa.

Msaada wa kibinadamu ukidondoshwa Gaza 12.March 2024
Ndege za kijeshi zikidondosha msaada wa kibinadamu Picha: Menahem Kahana/AFP

Na mtazamo huo umetolewa na mashirika 25 ikiwemo la haki za binadamu la Amnesty International na Oxfam,kupitia taarifa yao ya pamoja iliyotolewa jana Jumatano.  Katika mji wa Gaza City Wapalestina waliokata tamaa wameonekana wakisubiri kuwasili kwa boti ya msaada ya shirika la hisani la Open Arms.

Mkaazi mmoja kwa jina Eid Ayub amesema shirika hilo hupeleka msaada lakini unapowasili hakuna shirika la kusambaza. Lakini pia mkaazi huyo anasema msaada unasafirishwa kwa njia ya bahari na ule unaondondoshwa kwa madege hautoshi. 

Jumatano  pia waziri wa mambo ya nje wa Cyprus  Constantinos Kombos alisema meli nyingine ya pili ya msaada ambayo ni kubwa zaidi ilikuwa ikijiandaa kuelekea Gaza.Soma pia: Malori ya misaada ya WFP yawasili Gaza

Kombos pia alifanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mawaziri na maafisa wa ngazi za juu kutoka Uingereza,Umoja wa Falme za kiarabu,Qatar,Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa yaliyojikita katika suala la  njia ya baharini.

Wote walikubaliana njia bora zaidi kwa sasa ni ya barabara kupitia Misri na Jordan na kuingia Israel hadi Gaza.

Magari ya  UN yakiingiza  msaada wa kibinadamu Ukanda wa Gaza
Msafara wa magari ya UN ukiwa na msaada wa kibinadamuPicha: picture alliance/Anadolu

Kwa mtazamo huo pia wakaitaka Israel ifungue bandari ya Ashdood kaskazini mwa Gaza. Pamoja na juhudi hizo za kupelekwa msaada Gaza,bado Wapalestina katika eneo hilo wanaendelea kusubiri matokeo ya mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kusitisha vita.

Mpaka sasa juhudi hizo za upatinishi zimeshindwa kupata makubaliano mapya ya kusitisha vita na waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant ameapa kwa mara nyingine kwamba vikosi vya nchi hiyo vitaingia kila kona  ya Gaza kutimiza azma yao ya kuliangamiza kundi la Hamas.

Wakati huohuo Marekani inatarajiwa kutangaza vikwazo vipya kuhusiana na vituo viwili vilivyojengwa kinyume cha sheria na walowezi wa kiyahudi katika maeneo mawili ya Ukingo wa Magharibi.

Vituo hivyo vinatumika kama ngome za mashambulizi ya walowezi wa Israel wanaotajwa kuwa na itikadi kali. Vikwazo hivyo vinatarajiwa kutangazwa leo alhamisi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW