1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mo Dewji arejea nyumbani salama salimini

Zainab Aziz
20 Oktoba 2018

Mfanyabiashara maarufu wa nchini Tanzania aliyetoweka wiki iliyopita, Mohammed Dewji amepatikana na amerejea nyumbani salama salimini:

https://p.dw.com/p/36rj9
Tansania Mohammed Dewji, Geschäftsmann
Picha: Getty Images/AFP/K. Said

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Dewji amemshukuru Mungu, Watanzania na wote duniani waliomuombea apatikane salama na pia amelishukuru jeshi la polisi la Tanzania kwa kufanya kazi kuhakikisha anapatikana.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo Jumamosi, Inspekta Mkuu wa Polisi ya Tanzania Simon Sirro amesema Dewji alitelekezwa na watu waliokuwa ndani ya gari ambalo polisi ililionyesha kwa vyombo vya habari jana Ijumaa.

Silaha zapatikana

Simon Sirro  Polizeichef Dar es Salaam
IGP Simon Sirro, Inspekta Mkuu wa Polisi Tanzania (Picha ya Maktaba) Picha: DW/H.Bihoga

Sirro amesema baada ya kutelekezwa ''Mohammed Mo alipata mlinzi mmoja akapiga simu kwa wazazi wake, baadaye ndipo sisi tukapata taarifa na polisi wakawahi kwenye eneo la tukio.''

Inspekta Mkuu Sirro amesema watekaji walitaka kuliteketeza gari kwa moto kabla ya kukimbia lakini hawakufanikiwa, na kwamba ndani ya gari hilo polisi imekuta bunduki nne na risasi 19.

Kulingana na mkuu huyo wa polisi, waliokuwa wamemteka Mo Dewji walikuwa wakitaka kupatiwa fedha, na Mo amesema muda wote walionyesha kuwa na wasiwasi mkubwa.

Familia yashukuru

Awali leo, baba yake Mo, Gullam Dewji amethibitisha mwana wake amepatikana. Familia hiyo ilikuwa imetangaza kitita cha karibu dola nusu milioni kwa yeyote ambaye angetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa Mohamed Dewji ambaye ndiye bilionea mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika.

Dewji mwenye umri wa miaka 43, anaongoza kundi la makampuni ya METL ambayo yanahudumu katika zaidi ya nchi kumi yakiwekeza katika sekta za kilimo, bima, uchukuzi na vyakula. Inakadiriwa ana utajiri wa thamani ya dola bilioni 1.5.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Caro Robi