1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa AU na vyama vya wafanyakazi kujadili rushwa

George Njogopa10 Agosti 2018

Mkutano huo unajaribu kumulika ukubwa wa tatizo la rushwa barani Afrika na kuainisha njia bora zitakazosaidia kusafisha kadhia hiyo

https://p.dw.com/p/32z1W
Südafrika Protest gegen Korruption ARCHIV
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Umoja wa Afrika umekutana na Shirikisho la vyama vya wafanyakazi barani afrika nchini Tanzania kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na vitendo vya rushwa barani afrika tatizo ambalo linatajwa kuwa sugu katika mataifa mengi. 

Katika kikao chao cha siku tatu pande hizo zinajaribu kumulika ukubwa wa tatizo hilo na kuainisha njia bora zitakazosaidia kusafisha kadhia hiyo ambayo kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Transparency International tatizo la rushwa limemea mizizi karibu sehemu kubwa ya bara la Afrika.

Ingawa kumekuwa na juhudi kwa baadhi ya mataifa ya Afrika kuonyesha mikakati ya dhati kukabiliana na tatizo hilo, lakini kwa ujumla wake vigogo wa serikali, watumishi wa umma na wale wanaohusika na utoaji wa kandarasi za ujenzi na miradi mikubwa wanachukua sehemu kubwa ya rushwa inayotaja barani humu.

Ndoto ya kuiangamiza rushwa Afrika yakumbwa na changamoto

Wanaharakati nchini Kenya wakiandamana huku wamebeba mabango yenye ujumbe wa kupinga ufisadi
Wanaharakati nchini Kenya wakiandamana huku wamebeba mabango yenye ujumbe wa kupinga ufisadiPicha: picture alliance/dpa/D. Kurokawa

Katika mkutano huo ambao pia umewajumuisha washiriki kutoka mashirika ya kiraia, Tanzania ilitajwa kama moja ya nchi chache barani Afrika ambazo zimeonyesha utashi wa dhati kupiga vita vitendo vya rushwa.

Rais wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania Peter Tumaini Nyamhokya anayeshiriki mkutano huo amesema nchi za Afrika zimedhamiria kubadilishana ujuzi wa kupambana na vitendo vya rushwa.

Akizungumzia hali ya rushwa barani Afrika, mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu Onesmo Olengurumwa amesema licha ya utashi unaonyeshwa katika baadhi ya maeneo lakini ndoto ya Afrika kuimaliza kadhia hiyo bado inakabiliwa na kibarua kigumu.

Wajumbe kwenye mkutano huo kesho watatoa maazimio yao ya pamoja yatayoangazia njia zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri:Josephat Charo