1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLesotho

Mjadala wa Lesotho kutaka sehemu ya Afrika Kusini

31 Machi 2023

Wabunge wa Lesotho wanajadili hoja inayopendekeza kwamba taifa hilo lichukue maeneo makubwa wanayodai kuwa sehemu ya taifa lao, ilhali kwa sasa ni sehemu ya taifa jirani la Afrika Kusini. Je hilo litawezekana kweli?

https://p.dw.com/p/4PYYt
Global Ideas I Lesotho
Picha: Stefan Möhl/DW

Wachambuzi wanasema hata kama hoja hiyo itapitishwa na bunge la Lesotho, haitakuwa rahisi kwa jirani yake Afrika Kusini ambayo ina nguvu zaidi kijeshi na kiuchumi kuruhusu kipande chake chochote cha ardhi kupewa Lesotho.

Aidha, kuruhusu jambo kama hilo kufanyika ni kukiuka makubaliano ya miaka ya 1960 baina ya nchi za Afrika, kwamba zitaheshimu mipaka ya nchi zao kama ambavyo zimekuwepo tangu karne za unyonyaji wa mkoloni katika bara hilo.

Kulingana na hoja hiyo, maeneo kadhaa ya taifa dogo la kifalme Lesotho, yalichukuliwa na walowezi wa Uholanzi wakati wa msururu wa vita vya mipaka katika karne ya 19.

Hoja hiyo inapendekeza kuwa Lesotho ichukue jimbo la Free State la Afrika Kusini lenye ukubwa wa kilomita mraba 130,000. Ukubwa huo ukiwa ni mara nne zaidi kuliko taifa zima la Lesotho, na sehemu nyingine za mikoa mingine inayopakana na taifa hilo dogo.

Hoja hiyo inapendekeza kuwa Lesotho ichukue jimbo la Free State la Afrika Kusini lenye ukubwa wa kilomita mraba 130,000. Ukubwa huo ukiwa ni mara nne zaidi kuliko taifa zima la Lesotho, na sehemu nyingine za mikoa mingine inayopakana na taifa hilo dogo.
Hoja hiyo inapendekeza kuwa Lesotho ichukue jimbo la Free State la Afrika Kusini lenye ukubwa wa kilomita mraba 130,000. Ukubwa huo ukiwa ni mara nne zaidi kuliko taifa zima la Lesotho, na sehemu nyingine za mikoa mingine inayopakana na taifa hilo dogo.Picha: Stefan Möhl/DW

Wakaazi wengi wa maeneo hayo ni wa jamii sawa ya Basotho, ambayo huunda idadi jumla ya watu milioni mbili raia wa Lesotho. Takwimu zinaeleza kuwa idadi ya Wabasotho wa Afrika Kusini ni mara mbili zaidi kwa wingi kuliko Walesotho.

Hoja hiyo imewasilishwa na Tsepo Lipholo, kiongozi wa chama kidogo cha upinzani Basotho Convenient Movement ambaye ndiye mwakilishi pekee wa chama hicho katika bunge lenye viti 120.

Ni hoja inayojadiliwa mara kwa mara lakini si maarufu

Mnamo Jumatano, aliliambia bunge kwamba historia imenakili vyema ni nini kilichukuliwa kutoka Lesotho, watu wao waliuawa na kwamba muda umewadia wa kurekebisha maovu hayo na kurejesha kilichokuwa chao nchini mwao.

Kunyakuliwa kwa ardhi ya Basotho na walowezi wa Uholanzi ambao vizazi vyao, kwa sasa ndio wanamiliki sehemu kubwa ya ardhi ya jimbo la Free State, imenakiliwa vyema kwenye kumbukumbu za historia.

Mji wangu: Maseru Lesotho

Lesotho iliwekwa chini ya ulinzi wa Uingereza mwaka 1868, baada ya aliyekuwa mfalme kwa wakati huo Moshoeshoe, kuwaomba maafisa wa Uingereza kuzuia ardhi zao zisiendelee kuchukuliwa.

Mipaka ya nchi hiyo ikachorwa na mwaka uliofuata, mkataba ulisainiwa kati ya Uingereza na walowezi wa Uholanzi. Baadaye nchi hiyo ilimegwa na Uingereza kama koloni lake hadi ilipopata uhuru mwaka 1966.

Katika kampeni zake mwaka uliopita, Lipholo aliahidi kuyarudisha maeneo hayo. Anajenga hoja yake kwenye azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1962 lililotambua haki ya kujiamulia na kujitegemea kwa watu wa Basotho.

Eswatini pia hudai baadhi ya mashamba ya Afrika Kusini yalikuwa sehemu yake

Swali kuu linaloulizwa ni je itawezekana? Jibu ni haiwezekani.

Pendekezo hilo si maarufu hata miongoni mwa Walesotho ambao wanakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, umaskini, ukosefu wa ajira na visa vya uhalifu.

Mfalme Mswati III wa Eswatini pia amewahi kudai kuwa baadhi ya mashamba ya Afrika Kusini yalikuwa sehemu ya nchi yake.
Mfalme Mswati III wa Eswatini pia amewahi kudai kuwa baadhi ya mashamba ya Afrika Kusini yalikuwa sehemu ya nchi yake.Picha: Gulshan Khan/AFP/Getty Images

Japo ni suala linaloibuka mara kwa mara, halionekani kuungwa mkono na wengi bungeni kuweza kulipitisha kuwa sheria.

Katika miaka ya nyuma, Mfalme Mswati III wa Eswatini, pia aliibua mjadala kama huo akidai kwamba kihistoria, baadhi ya mashamba makubwa makubwa ya Afrika Kusini yalikuwa sehemu ya taifa lake na kutaka yarudishwe. Hata hivyo, madai hayo hayajatekelezwa.

Mnamo mwaka 1964, viongozi wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU, ambao kwa sasa ni Umoja wa Afrika waliafikiana mjini Cairo, Misri, kwamba nchi zao zitatambua mipaka waliyorithi kutoka kwa wakoloni wao ili kuzuia migogoro ya siku za baadaye.

Kwa mantiki hiyo, Afrika Kusini ina sababu ya dhati kuyapinga madai ya jirani yake.

Chanzo: RTRE