1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa kihistoria wa televisheni nchini Misri

11 Mei 2012

Wamisri wamejionea tukio la aina pekee katika historia ya nchi yao:Mjadala wa kwanza wa televisheni kati ya wagombea wawili wa kiti cha urais, Amr Moussa na Abdel Moneim Aboul Fotouh.

https://p.dw.com/p/14tl1
Amr Moussa na Abdel Abu Futuh katika mjadala wao wa televisheniPicha: picture-alliance/dpa

Miezi 15 baada ya wanamapunduzi wa uwanja wa Tahrir  kumn'goa madarakani Mohammed Hosni Mubarak, wamisri wamefuatilizia kwa muda wa masaa manne majadiliano moto moto kati ya Amr Moussa, mwanadiplomasia aliyekomaa mwenye umri wa miaka 75, aliyetumikia utawala wa Mubarak, na Abdel Moneim Aboul Fotouh, mfuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam, mwenye umri wa miaka 60, na ambae alitumikia kifungo jela wakati wa utawala wa rais wa zamani.

Kati ya wagombea 13 walioorodheshwa, hawa wawili ndio wanaopewa nafasi nzuri ya kufanya vyema katika uchaguzi huo wa rais ambao duru ya kwanza itaitishwa May 23 na 24 mwaka huu. Duru ya pili itaitishwa mwezi ujao. Uchaguzi huo wa urais utakamilisha kipindi cha mpito kinachoongozwa na baraza kuu la wanajeshi tangu mapinduzi ya uwanja wa Tahrir.

Mjadala huo ulioonyeshwa moja kwa moja na vituo viwili vya kibinafsi vya televisheni, umefuatiliziwa katika nchi zote za ulimwengu wa kiarabu.

Ägypten Kairo Freitagsgebet Tahier Platz
Waumini wasali sala ya ijumaa katika uwanja wa Tahrir mjini CairoPicha: Reuters

Wagombea hao wawili walijaribu kila mmoja kumnasa mwenzake lilipohusika suala kwa mfano la nafasi ya sharia ya kiislam au uhusiano pamoja na Israel.

Aboul Fotouh, aliyewahi kuwa mwanachama wa Udugu wa kiislamu, kila wakati alikuwa akikumbusha enzi za Amr Moussa katika utawala wa zamani anaosema "umeifisidi Misri."

"Wahenga wanasema-"aliyezusha tatizo hawezi kulifumbua"-amesema Aboul Fotouh. Mpinzani wake amejitetea akihoji mapinduzi yalipowadia,alikuwa akiongoza Umoja wa Nchi za Kiarabu-Arab League- na kwamba hakuwa tena waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri tangu mwaka 2001.

Amewatuhumu wafuasi wa Udugu wa kiislam kwa kukaa kimya muda wote.-"Unapigania masilahi ya Udugu wa kiislam na sio ya Misri" amesema mwanadiplomasia hiyo.

Wagombea wote wawili wameahidi kuyadurusu maakubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 1979 pamoja na Israel- nchi ambayo Aboul Fotouh anaitaja kuwa ni adui, huku Amr Moussa akiita kuwa "mshindani".

Kamal Ganzouri und Mohamed Hussein Tantawi Kairo Ägypten
Waziri mkuu Kamal Ganzouri na mkuu wa baraza la kijeshi la mpito Mohamed Hussein TantawiPicha: picture-alliance/dpa

Uchaguzi wa kwanza wa kweli wa urais katika nchi hiyo yenye wakaazi  zaidi ya milioni 80 unaangaliwa katika eneo lote la mashariki ya kati kama kipimo cha mageuzi yanayotokana na kilio cha umma kilichohanikiza mwaka jana.

Zoezi la kupiga kura linaanza leo kwa wamisri karibu laki sita wanaoishi katika nchi 166 kumchagua yule wanaetaka aiongoze nchi yao siku za mbele.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa

Mhariri:  Miraji Othman