Misri, Sudan, Ethiopia zashindwa kuafikiana kuhusu bwawa | Matukio ya Afrika | DW | 10.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Misri, Sudan, Ethiopia zashindwa kuafikiana kuhusu bwawa

Bado hakuna maafikiano kati ya Misri, Sudan na Ethiopia juu ya mzozo kuhusu bwawa kubwa la umeme linalojengwa katika mto Nile licha ya mazungumzo ya siku mbili.

Misri, Sudan na Ethiopia zimeshindwa kufikia muafaka baada ya mazungumzo ya siku mbili juu ya mzozo kuhusu bwawa kubwa la umeme linalojengwa na Ethiopia kwenye mto Nile.

Hata hivyo Misri imesema inayo matumaini kuwa makubaliano yatapatikana kabla ya tarehe 15 Januari, ambayo ni muda wa mwisho waliokubaliana na Marekani.

Waziri wa maji wa Misri Mohammed Abdel Aty amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa, kwamba nchi hizo zimeweza angalau kukubaliana juu ya masuala muhimu, likiwemo lile la namna ya kulijaza maji bwawa hilo linalojengwa na Ethiopia.

Hata hivyo, mwenzake wa Ethiopia Sileshi Bekele, ameishutumu Misri kuja kwenye meza ya mazungumzo bila nia ya kufikia makubaliano.

Wajumbe wa nchi hizo tatu watakutana tena mjini Washington Januari 13, ambapo waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin na rais wa Benki ya Dunia Davis Malpass watashiriki.