Miili ya Waafrika iliyopelekwa Ulaya kwa utafiti yazikwa
24 Machi 2026
Mabaki ya kiasi watu 63 wa jamii za Khoi na San yalikuwa yamerejeshwa kutoka kwenye jumba moja la makumbusho la Ulaya, ikiwa ni sehemu ya harakati pana barani Afrika ya kuleta mabaki na vitu vya kale vilivyoibwa au kuondolewa barani humo.
Wakitambuliwa sana kama wakaazi wa mwanzo kabisa kusini mwa Afrika, Wakhoi na Wasan walipigana dhidi ya ukoloni, na wengi waliuawa na walowezi wa Ulaya. Mabaki yaliyozikwa upya yalichimbwa kati ya mwaka wa 1868 na 1924 na kuwekwa katika Jumba la Makumbusho la Hunterian katika Chuo Kikuu cha Glasgow huko Scotland.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye alihudhuria mazishi hayo pamoja na wawakilishi wa makumbusho na viongozi wa kitamaduni, alisema kurejeshwa kwa mabaki hayo kulifuatia mazungumzo kati ya chuo kikuu hicho na serikali yaliyoanza mwaka wa 2022.