1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali itajiuzulu ikiwa wananchi watayaunga mkono mageuzi

Admin.WagnerD2 Julai 2015

Rais wa Ufaransa Hollande amesema ikiwa Wagiriki watapiga kura ya kuiunga mkono sera ya mageuzi iliyopendekezwa na wakopeshaji wa kimataifa, mpango mpya wa kuikoa Ugiriki utaweza kupatikana haraka.

https://p.dw.com/p/1FrvD
Griechenland Athen Schuldenkrise
Picha: Reuters/Y. Behrakis

Watu wa Ugiriki watashiriki katika kura ya maoni jumapili ijayo,ili kuamua juu ya sera hiyo ya kubana matumizi iliyopendekezwa na wakopeshaji wa kimataifa. Pande tatu ambazo mpaka sasa zimekuwa zinautekeleza mpango wa kuiokoa Ugiriki zinaitaka serikali ya nchi hiyo iyakubali mapendekezo ziliyoyatoa ili nchi hiyo ipatiwe mikopo mingine.

Lakini serikali ya Ugiriki inafanya kampeni ili wanachi wayakatae mapendezo ya pande hizo, yaani Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya ECB. Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amesema wagiriki watapiga kura ya kuamua juu ya mustakabali wa nchi yao na siyo tu juu ya kuwamo katika Euro. Amesema siku ya jumapili "tutaamua baina ya kuukubali mpango huu wa uokozi na kutafuta suluhisho zuri "

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis
Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis VaroufakisPicha: Reuters/Y. Herman

Wastaafu wamuunga mkono Waziri Mkuu

Waziri Mkuu Tsipras amesema ameyakataa mapendekzo ya wakopeshaji wa kimataifa kwa sababu yanalenga shabaha ya kuyakata mafao ya uzeeni. Waziri Mkuu Tsipras anaungwa mkono na baadhi ya wastaafu. Mmoja wao amesema watu wa Ugiriki wanataka kuendelea kuwamo katika sarafu ya Euro, lakini siyo chini ya masharti ambayo mataifa ya Ulaya yenye nguvu kubwa yanawalamizisha wagiriki wayakubali.

Lakini Waziri wa fedha Yanis Varoufakis amesema leo kwamba ikiwa wananchi wa Ugiiki wataamua kuiunga mkono sera ya kubana matumizi katika kura ya maoni Jumapili ijayo serikali itajiuzulu.Amesema itafanya hivyo kwa moyo wa ushirikiano na yeyote atakaeyachukua mamlaka ya serikali

Hata hivyo mwenyekiti wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro,Jeroen Dijssselbloem amesema itakuwa vigumu sana kuutayarisha mpango mpya wa kuiokoa Ugiriki, ikiwa wagiriki wataamua kuyakataa mapendekezo ya wadai wa kimataifa katika kura ya maoni ya Jumapili ijayo.

Mkuu wa kundi la Euro Jeroen Dijsselbloem.
Mkuu wa kundi la Euro Jeroen Dijsselbloem.Picha: Reuters/Y. Herman

Akihutubia kwenye kamati ya Bunge, Dijsselbloem ameuliza patakuwapo na msingi gani wa umiliki ikiwa wagiriki watasema hapana katika kura ya maoni? Dijsselbloem ambae pia ni waziri wa fedha wa Uholanzi amesema mambo yatakuwa magumu sana na ameilaumu serikali ya Ugiriki kwa kuendesha kampeni ya kuwahimiza wagiriki wapige kura ya hapana.

Lakini Waziri wa uchumi wa Uhispania Luis de Guindos amesema mlango wa mazungumzo utakuwa wazi bila ya kujali matokeo ya kura ya maoni.Lakini wakati huo huo ametahadharisha juu ya madhara yanayoweza kutokea ikiwa wagiriki watapiga kura ya hapana. Amesema yumkini Ugiriki italazimika kujiondoa kwenye sarafu ya Euro, jambo ambalo amesema hakuna anaetaka kuliona.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga