1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfahamu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Mohammed Khelef Amina Mjahid
1 Novemba 2025

Rais Samia Suluhu Hassan ametangazwa mshindi wa kiti cha urais, baada ya kujizolea asilimia 98 ya kura katika uchaguzi wa Oktoba 20 uliojaa vurugu. Matokeo hayo yalitangazwa na Tume huru ya uchaguzi nchini humo INEC.

https://p.dw.com/p/52l6y
Tanzania 2025 | Samia Suluhu Hassan
Rais anaetetea kiti chake Samia Suluhu Hassan Picha: AP/picture alliance

Rais Samia ambae ni mama wa watoto wanne, mzaliwa wa Zanzibar, na mwanasiasa aliyeingia kwenye ulingo wa siasa akitokea makundi ya asasi za kijamii. Samia Suluhu Hassan alishika nafasi ya urais mnamo mwezi Machi 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, ambaye alihudumu kama makamu wake kwa kipindi cha miaka mitano ya awali.

Mwenyekiti huyo wa chama kinachotawala, CCM, ana umri wa miaka 65 akiwa amesomea uchumi katika ngazi ya shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe nchini Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani.

Safari ya Samia ilianza kwa kuwa mbunge wa viti maalum

Kabla ya kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu, mama huyo wa watoto wanne alikuwa mbunge wa viti maalum baina ya mwaka 2000 na 2005 na baadaye mbunge wa kuchaguliwa wa jimbo la Makunduchi la kusini Unguja kutoka mwaka 2010 hadi 2015.

Ghasia za baada ya uchaguzi Tanzania,Mtihani kwa rais Samia

Awali alikuwa waziri katika wizara mbalimbali visiwani Zanzibar kabla ya kuchaguliwa kuwa waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na baadaye kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba.

Kwenye kampeni za mwaka huu, Samia alizungumzia uendelezaji wa miradi ya miundombinu, huduma za afya, elimu na ajira kwa vijana. Rais huyo, ambaye awali alipoingia madarakani alikuwa ameanza kujijengea sifa ya kuirejesha nchi kwenye maridhiano ya kisiasa, ameahidi pia kuuendeleza mchakato huo na pia kuanzisha utaratibu wa katiba mpya.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi