Merkel achaguliwa tena kuongoza CDU | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel achaguliwa tena kuongoza CDU

CDU hakiwezi kuingia kwenye serikali ya muungano na SPD wala Wanamazingira (Greens)

default

Kansela Angela Merkel akizungumza katika mkutano wa CDU

Kansela Angela Merkel amewaonya wafuasi wa chama chake kwamba nafasi ya Ujerumani, kimataifa, inaelekea mashakani na kuwashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kukataa kwenda na wakati. Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama chake hii leo huko Karlsruhe, amekitaka pia  chama chake cha Christian Demokratic, CDU,  kuunga mkono mpango wa kupunguza bajeti ya shughuli za ulinzi miongoni mwa mambo mengine.

Kansela Angela Merkel aliyechaguliwa tena kukiongoza chama hicho ameuhutubia mkutano mkuu wa chama chake cha CDU wakati chama hicho kikitazamiwa kubadilisha mtazamo wake wa kale wa kuunga mkono mpango wa lazima wa  kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana nchini Ujerumani, pamoja na kuidhinisha hatua za kupunguza bajeti ya kijeshi.

Katika hotuba yake ya dakika 75 iliyoshangiliwa sana na wanachama wa CDU katika mkutano hu, kiongozi huyo wa Ujerumani amejibu ripoti za vyombo vya habari na msimamo wa wanasiasa wa mrengo wa kati kulia wa kuikosoa serikali yake katika suala la kuwajumuisha wageni nchini, akisema wale watakaoshindwa kujumuika katika jamii ya Wajerumani watakabiliwa na hali ngumu.

Ama kwa upande mwingine, amepinga maoni yaliyojitokeza hivi karibuni kwamba chama chake huenda kikajikuta siku moja kinarudi tena katika  serikali ya muungano na chama cha Social Demokratic SPD au chama cha kijani.

CDU-Parteitag - Übersicht, Merkel

Wanachama wa CDU

Aidha katika masuala ya kimataifa amekiri mbele ya mkutano huo kwamba China imechukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Ujerumani ya kuongoza kibiashara duniani, akiongeza kusema kwamba idadi ya Wajerumani inapungua kwa kasi kubwa kabisa. Kazi kubwa ya chama chake cha CDU amesema ni kuisaidia Ujerumani kwenda na mabadiliko ya dunia na kuandaa mkondo wa baadae wa taifa hili. 

Akitolea mfano mkutano wa kilele wa nchi za G20 uliofanyika wiki iliyopita huko Korea Kusini, ambako aliipinga miito ya kuitaka nchi yake iweke vipimo katika nakisi ya shughuli za kibiashara, amekiambia chama chake kwamba hawatokubali kuadhibiwa kutokana na ukweli kwamba Ujerumani inatengeneza  bidhaa bora.

Ametoa mwito wa chama chake kuunga mkono miradi mikubwa ili kuiendeleza mbele  nchi, akinadi kwamba hakuna mazuri yanayokuja bila ya juhudi. Kwa maneno yake, bibi Merkel amekiri kwamba kwa mtu yoyote aliyewahi kwenda China au Korea Kusini anaweza kusema wazi kuwa ulimwengu haujalala.Kutokana na hilo amewashambulia wapinzani wa CDU, SPD  pamoja na Wanamazingira kwa kupinga mageuzi muhimu nchini. 

Ameelekeza lawama pia kwa Kansela wa zamani, Gerhard Schroeder, kutoka chama cha SPD pamoja na aliyekuwa waziri wake wa Fedha, Hans Eichel, kwa kuikubalia Ugiriki kujiunga na kundi linalotumia sarafu ya Euro. Pia amekishutumu chama hicho kwa kucheza mchezo mbaya wa kijibadilisha rangi kama kinyonga kutokana na hatua yake ya kuidhinisha  usafirishaji  wa  takataka za nuklia  wakati walipokuwa serikalini na kuikosoa hatua hiyo wakati wameingia kwenye upinzani.

Mkutano huo mkuu wa chama cha CDU unaofanyika Karlsruhe Kusini Magharibi mwa Ujerumani utamalizika kesho.

Mwandishi: Saumu Yusuf/dpa/Reuters

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 15.11.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Q9lr
 • Tarehe 15.11.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Q9lr
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com