Membe kuwania urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo | Matukio ya Afrika | DW | 17.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Membe kuwania urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo

Aliyekuwa waziri wa Mambo ya Kigeni nchini Tanzania, Bernard Membe ametangaza kuwa atawania kiti cha urais wa Tanzania kupitia chama cha upinzani ACT-Wazalendo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka 2020.

Tansania Opposition Bernard Membe und Maalim Seif Sharif Hamad

Bernard Membe (kushoto) na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe

Akiandika kupitia ukurasa wa Twitter siku moja tangu alipokaribishwa kuwa mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo, Membe amesema amekubali kupeperusha bendera ya chama hicho na kuongeza kuwa yuko tayari kushiriki mazungumzo na vyama vingine vya upinzani kupata mgombea mmoja.

Membe amedokeza kuwa sasa ni wakati muafaka wa kufanya mashauriano na vyama vya upinzani ikiwemo chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA ili kusimamisha kile alichokiita ''Kisiki cha Mpingo'' kumaanisha mgombea mmoja imara wa upande wa upinzani.

Mwanadiplomasia huyo wa siku nyingi alivuliwa uanachama wake kutoka chama tawala CCM mapema mwaka huu kwa madai ya kukiuka kanuni za chama.

Wakati wa mkutano maalum wa kumkaribisha ndani ya chama cha ACT-Wazalendo uliofanyika siku ya Alhamisi (16.08.2020) Membe alisema kufukuzwa kwake kunatokana na uamuzi wa kutangaza nia ya kuwania urais ndani ya CCM na kutoa changamoto kwa rais aliye madarakani na anayesaka muhula wa pili John Magufuli.

''Kilichonivutia kujiunga na ACT-Wazalendo ni katiba ya chama na falsafa yake ya kutaka kuona mabadiliko katika utawala wa nchi'', alisema Membe wakati akizungumza na wafuasi wa ACT-Wazalendo waliohudhuria halfa ya kukaribishwa kwake.

Akitolea mfano wa kilichotokea hivi karibuni nchini Malawi, Membe alisema iwapo vyama vya upinzani vitaungana katika uchaguzi unaokuja, vitaweka uhakika wa kushinda uchaguzi na kushika hatamu za uongozi.