Mazungumzo kuhusu Ukraine yafanyika Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo kuhusu Ukraine yafanyika Berlin

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Ukraine wamemaliza mazungumzo kuhusu mzozo wa Ukraine Berlin bila ufanisi mkubwa. Mazungumzo hayo yalifanyika jana (17.08.2014) huku mapigano yakiendelea mashariki mwa Ukraine.

Mazungumzo ya Berlin kati ya mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka Urusi, Ukraine, Ujerumani na Ufaransa yaliyolenga kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Ukraine uliodumu kwa miezi minne, yalikamilika bila matokeo muhimu. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, alisema baada ya kikao hicho kilichodumu muda wa masaa matano kati yake na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, Pavlo Klimkin wa Ukraine na Laurent Fabius wa Ufaransa, kwamba mazungumzo yalikuwa magumu.

"Mazungumzo yalikuwa magumu lakini nadhani na natumai kumekuwa na ufanisi kuhusu masuala kadhaa. Tumekubaliana kwanza kuripoti kwa wakuu wetu wa nchi na baadaye siku ya Jumanne tukubaliane jinsi tutakavyoyaendelea mazungumzo haya ya leo."

Hata hivyo waziri Steinmeier hakufafanua aina ya ufanisi uliopatikana, lakini akasisitiza umuhimu wa kuepusha makabiliano zaidi kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine. Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mkutano huo uliofanyika nje kidogo ya mji mkuu Berlin baada ya wenzake kuondoka, Steinmeier alisema yalikuwa mazungumzo muhimu yaliyofanyika wakati mgumu.

Steinmeier aidha alisema yalikuwa mazungumzo ya uwazi na yaliyolenga njia za kufikia makubaliano ya kukomesha mapigano na kuimarisha udhibiti wa mpaka kati ya Urusi na Ukraine, pamoja na jinsi ya kuwapelekea watu misaada ya kibinadamu. "Lengo letu linabaki bila shaka kuchangia kufikia makubaliano ya usitishwaji mapigano nchini Ukraine kupitia uwezo wetu na kuepusha maafa zaidi katika siku zijazo kadri iwezekanavyo."

Mapigano mashariki mwa Ukraine

Mapigano kati ya vikosi vya Ukraine na waasi yaliendelea mashariki mwa Ukraine hapo jana hivyo kuzidi kuyadidimiza matumaini ya kuepusha vita kati ya Urusi na Ukraine. Mapiganao makali yalishuhudiwa katika eneo hilo kati ya vikosi vya serikali na waasi huku jeshi la Ukraine likisema ndege yake ya kivita chapa MiG ilidunguliwa karibu na mji wa Luhansk na rubani wa ndege hiyo akaruka kwa mwavuli kujisalimisha.

Lugansk Militärflugzeug abgeschossen

Ndege ya kijeshi iliyodunguliwa

Jeshi lilisema limepandisha bendera ya taifa katika kituo cha polisi cha wilaya katika kitongoji cha kaskazini mashariki mwa mji wa Luhansk baada ya mapigano makali na wanamgambo siku ya Jumamosi.

Wakati haya yakiarifiwa maafisa katika mji uliozingirwa wa Donetsk wamesema raia 10 wameuwawa na wengine 24 kujeruhiwa kwenye mashambulizi ya makombora katika saa 24, wakati vikosi vya serikali vilipoendelea kupambana na waasi walionasa mjini humo.

Msaada bado umekwama

Kwa upande mwingine Urusi na Ukraine zimeendelea kuvutana kuhusu msafara wa malori ya Urusi yaliyoegeshwa karibu na mpaka wa Ukraine yakiwa yamesheheni msaada, huku maafisa wakisema ukaguzi wa malori kiasi 300 haungeweza kuanza jana.

Russischer Konvoi mit Hilfsgütern für die Ukraine 14.08.2014

Msafara wa malori ya misaada ya Urusi

Kamati ya shirika la msalaba mwekundu inayosimamia usambazaji wa msaada huo ilisema maafisa wa Urusi na Ukraine wamekubaliana kuhusu taratibu za kuzikagua shehena za misaada hiyo inayoelekea Luhansk, lakini imesisitiza hakikisho la usalama linahitajika kuhusu jinsi malori hayo yatakavyovuka maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Muangalizi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, Paul Picard, aliliambia shirika la habari la AFP akiwa mpakani kwamba kutafanyika mkutano leo kati ya pande zote husika.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alimwambia makamu wa rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumamosi kuwa waasi wanasubiriwa watoe hakikisho kwamba msaada huo utapita salama katika maeneo yao. Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imeitaka Ukraine mara kadhaa isitishe mapigano ili msaada uweze kuwafikia raia katika miji ya mashariki mwa Ukraine, ambao wamenasa kwa siku kadhaa bila maji wala umeme.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/REUTERS

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com