Matokeo ya uchaguzi yasubiriwa Brazzaville
16 Machi 2026
Kura zimeendelea kuhesabiwa katika Jamhuri ya Kongo baada ya uchaguzi,wa rais ulioshuhudia idadi ndogo ya wapiga kura. Rais Denis Sassou N'Guesso anatarajiwa kushinda muhula wa tano.
Kura zilianza kuhesabiwa tangu jana baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa saa kumi na mbili jioni na matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa kati ya saa 48 hadi 72, wakati matokeo rasmi yakitarajiwa ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Imeelezwa kwamba idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa ndogo huku wakaazi wengi wakisema hawaamini uchaguzi huo utatowa matokeo yatakayoleta mabadiliko ya uongozi katika nchi ambayo imekuwa ikiongozwa kwa miaka 42 na rais mmoja Denis Sassou Nguesso.
Pamoja na kwamba upinzani ulitowa mwito wa kuususia uchaguzi huo vyama viwili vikubwa vya upinzani pekee ndivyo vilivyokaa pembeni wakati wagombea sita wengine walijitokeza kupambana kwenye uchaguzi huo na rais wa sasa mwenye umri wa miaka 82.
Hata hivyo wachambuzi wanasema hakuna kati ya wapinzani waliojitokeza kwenye uchaguzi huo anayeweza kuwa mshindani wa maana wa kumpa changamoto kiongozi huyo.
Lakini pia wapiga kura inaonesha tayari wanamjuwa mshindi na jambo muhimu wanalolitaka kwa atakayetangazwa mshindi ni kuweka mbele maslahi ya wananchi, kama anavyosema Marieete Makalebo mpiga kura wa Brazzavile.
"Mgombea atakayetangazwa anapaswa kutanguliza mbele maslahi ya wananchi. Watu wanapaswa kuwekwa mbele na hiyo ni kusema masuala ya kijamii yatangulizwe na hilo ndio muhimu''
Mawasiliano ya mtandao yalizimwa kote nchini humo kama ilivyo kawaida wakati wa chaguzi za rais huku usafiri wa magari pia ukidhibitiwa katika mji mkuu Brazzaville. Pamoja na mazingira hayo wachambuzi wanasema kugawika kwa upinzani na kudhibitiwa kwa taasisi za uchaguzi hakuna uwezekano wowote wa kuzuka machafuko, na wananchi pia wamekuwa wakisisitiza amani.
"Sote tunajuwa kwamba baada ya chaguzi siku zote kuna mambo ya hapa na pale lakini sisi tunataka amani. Hatutaki mapigano wala mivutano. Tunataka nchi yetu isonge mbele katika msingi mzuri. Hatutaki vita, tunataka rais mpya ajaekuleta mabadiliko hapa kwetu Congo''
Vyama viwili vilivyoususia uchaguzi vimedai yamekuweko mazingira ambayo hayawezi kutenda haki katika uchaguzi. Sassou Nguesso anagombea kupitia chama cha Congolese Party of Labor na aliingia madarakani mnamo mwaka 1979 hadi 1992 ambapo aliitisha kwa mara ya kwanza uchaguzi wa vyama vingi, alioshindwa na baadae akarejea tena madarakani kama kiongozi wa wapiganaji kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 1997.Mataifa ya Afrika ya Kati yachukulia vipi mapinduzi Gabon ?
Kura ya maoni ya katiba ikaondowa ukomo wa umri na mihula hatua iliyomfanya kugombea na kuendelea kubakia madarakani.
Congo Brazzavile inakabiliwa na madeni makubwa na taasisi za kimataifa yakifikia asilimia 94 ya pato jumla la nchi hiyo kwa mujibu wa benki ya dunia.
Pamoja na utajiri wake wa mafuta almasi na shaba, nusu ya idadi ya wakaazi wake takribana milioni 6 wanaishi kwenye umasikini.